
Wizara ya Elimu ya Korea Kusini imetangaza kuwa, skuli 4,008 za msingi, za kati na sekondari zimefungwa kote nchini humo kutokana na kupungua kwa kasi idadi ya wanafunzi, huku mamia ya taasisi za elimu na mafunzo zikibaki bila ya matumizi.
Kwa mujibu wa gazeti la Straits Times, takwimu za Wizara ya Elimu zilizotolewa na Jin Soon-mi, mwakilishi wa Chama tawala cha Kidemokrasia zinaonyesha kuwa, kati ya skuli zote zilizofungwa, 3,674 ni za msingi, 264 za elimu ya kati na 70 za sekondari; na kuonyesha kuwa sehemu kubwa ya skuli zilizofungwa ni za msingi.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, skuli 158 zimefungwa nchini Korea Kusini, na inatabiriwa kuwa skuli zingine 107 zitafungwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo kutokana na kupungua kwa idadi ya wanafunzi. Mwenendo huo ni mkubwa zaidi hususan katika maeneo yasiyo ya mijini na umezusha changamoto kubwa kwa muundo wa elimu wa nchi hiyo.
Kati ya skuli 4,008 zilizofungwa, vituo 376 vya elimu havijawahi kutumika; ambapo kati ya hizo, skuli 266 zimeachwa kwa zaidi ya miaka 10 na 82 kwa zaidi ya miaka 30.
Jin Soon-mi amesisitiza: “kadiri idadi ya wanafunzi inavyoendelea kupungua, ndivyo ufungwaji wa skuli utavyoendelea, na ramani ya njia ya muda mrefu inahitaji kutengenezwa ili skuli hizi zitumike kama mali kwa jamii za wenyeji.”
Kupungua kwa idadi ya wanafunzi kumesababisha pia mabadiliko makubwa katika muundo wa elimu wa Korea Kusini.
Wizara ya Elimu ya nchi hiyo ilitangaza mnamo mwezi Februari mwaka huu kwamba nafasi 2,232 za usomeshaji zimepunguzwa kwa mwaka wa masomo wa 2025 zikijumuisha walimu 1,289 wa skuli za msingi na walimu 1,700 wa skuli za kati.
Changamoto hiyo iliyoikumba Korea Kusini imechangiwa na kutokuwepo ongezeko la idadi ya watu, hali inayoelezewa kama kengele ya hatari kwa mustakabali wa nchi hiyo…/