Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald Trump wa Marekani na Volodymyr Zelensky wa Ukraine, wamesema kuna maendeleo
yamepatikana katika mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine wakati wa
mazungumzo ya Florida lakini rais wa Marekani amekiri kwamba tatizo la mpaka
bado “halijatatuliwa.”
Akihutubia waandishi wa habari huko Mar-a-Lago, Zelensky
alisema wamefikia makubaliano kuhusu “90%” ya mpango wa amani wa vipengele
20, huku Trump akisema dhamana ya usalama kwa Ukraine “imekamilika karibu
95%.
Baadaye Zelensky alisema timu za Marekani na Ukraine
zitakutana wiki ijayo kwa mazungumzo zaidi kuhusu masuala yanayolenga kukomesha
vita vya Urusi vilivyodumu kwa karibu miaka minne nchini Ukraine.
“Tulikuwa na mazungumzo muhimu kuhusu masuala yote na
tunathamini maendeleo ambayo timu za Ukraine na Marekani zimepiga katika wiki
zilizopita,” Zelensky alisema katika taarifa ya Telegram.
Pendekezo la kugeuza eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine,
ambalo Urusi kwa kiasi kikubwa inalidhibiti, kuwa eneo lisilo la kijeshi bado “halijatatuliwa,” Trump alisema.
Moscow kwa sasa inadhibiti takriban 75% ya eneo la Donetsk,
na takriban 99% ya eneo jirani la Luhansk. Mikoa hiyo kwa pamoja inajulikana
kama Donbas.
Urusi inataka Ukraine ijiondoe kutoka sehemu ya eneo ambalo
bado inalidhibiti huko Donbas, huku Kyiv ikisisitiza kuwa eneo hilo linaweza
kuwa eneo huru la kiuchumi linalolindwa na vikosi vya Ukraine.
Urusi ilianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine Februari 2022, na
kwa sasa Moscow inadhibiti takriban 20% ya eneo la Ukraine.
Pia unaweza kusoma: