Chanzo cha picha, Reuters/ Social
-
- Author, Bushra Mohamed
- Nafasi, BBC
-
Muda wa kusoma: Dakika 4
Tangu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu atangaze nchi yake kuitambua Jamhuri ya Somaliland, eneo la Somalia lililojitangazia uhuru wake, miito ya kimataifa ya kuunga mkono serikali ya Somalia imekuwa ikiongezeka.
Waziri Mkuu Netanyahu aliposaini hati ya utambuzi wa Somaliland, alimwambia Rais wa Somaliland, Abdirahman Mohamed Abdillahi Irro, kwa simu kwamba atamjulisha Rais Donald Trump wa Marekani, kuhusu hamu ya Somaliland ya kujiunga na Makubaliano ya Abraham watakapokutana.
{Makubaliano ya Abraham (Abraham Accords) ni makubaliano yanayosimamiwa na Marekani, kuanzia mwaka 2020, ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu, nchi ambazo tayari ziko katika makubaliano hayo ni pamoja na UAE, Bahrain, Morocco, Sudan.}
Gazeti la New York Post nchini Marekani liliripoti kwamba Rais wa Marekani Donald Trump aliulizwa ikiwa ataitambua Somaliland kufuatia uamuzi wa Israel, gazeti hilo limeripoti kuwa kiongozi huyo “hayuko tayari kuitambua Somaliland.”
Israel na Somaliland zinafaidika nini?
Chanzo cha picha, Wikipedia
Bado haijulikani Somaliland ambayo mji mkuu wake ni Hargeisa, imetoa nini ili kutambuliwa na Tel Aviv, na kuifanya Israel kuwa nchi ya kwanza duniani kuitambua.
Lakini inaeleweka kuwa Somaliland iko kwenye njia muhimu ya bahari, Bahari ya Shamu na lango la Bab al-Mandab, ambapo asilimia thelathini ya biashara ya dunia hupitia.
Wachambuzi wanaamini moja ya sababu ya Israel kuitambua Somaliland ni uwepo wa nchi hiyo katika eneo hilo, hasa katika Bahari ya Shamu, ambapo meli zake za kibiashara zimeshambuliwa mara kadhaa.
Ingawa haijatangazwa rasmi, serikali ya Somalia imesema haitakubali kamwe Israel kuanzisha kambi ya kijeshi ndani ya Somalia.
Usalama, ambao ndio wasiwasi mkubwa wa Israel, ndilo jambo ambalo wachambuzi wa kikanda wanaamini Somaliland inaweza kushirikiana ya Israel.
“Bila shaka, ni muhimu kwa Israel kuanzisha uhusiano na Somaliland, ili kupambana na nchi au makundi adui, hasa Wahouthi na Iran,” anasema Martin Plaut, mtaalamu wa masuala ya Pembe ya Afrika.
Ameongeza kuwa Israel imekuwa ikijitahidi kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi katika eneo hilo, hasa zile za Kiislamu na Kiarabu.
Israel imefanya uvamizi katika Ukanda wa Gaza kwa miaka miwili iliyopita, vita ambavyo pia vimesababisha makabiliano na Iran na kundi la Houthi. Kuna mtazamo kwamba Israel kuitambua Somaliland kunaweza kuwa na matokeo mabaya ya usalama kwa Somaliland.
“Kuna hofu ya kutokea kwa vitendo vinavyoweza kutishia usalama wa Somaliland kutoka kwa Wahouthi. Pia kuna nchi ambazo ni wapinzani wa Israel, ikiwa ni pamoja na Uturuki, ambazo zinaweza kufanya vitendo vinavyoweza kudhoofisha muungano wa Somaliland na Israel,” amesema Abdifatah Tahir, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.
Vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti mapema mwaka huu kwamba Ankara inataka kuanzisha kambi ya satelaiti ndani ya Somalia, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wamelitaja kama sababu ya Israel nayo kutaka kuingia Somaliland, kutokana na ushindani kati ya nchi hizo mbili.
Tahir anaongeza kuwa utambuzi huo utaleta faida kwa Somaliland, kwani Israel ndiyo nchi ya kwanza kuitambua na kuunda uhusiano wa kidiplomasia.
“Israel ni nchi yenye idadi kubwa ya Wayahudi, wenye jamii zenye nguvu nje ya nchi, na ushawishi wa kisiasa na kiuchumi. Inatarajiwa kwamba kikosi hiki kitashawishi nchi zingine kuitambua Somaliland,” aliongeza.
Bado kuna nchi nyingi duniani ambazo zimetambuliwa na nchi zingine, ikiwa ni pamoja na Kosovo, lakini bado hazijawa wanachama wa Umoja wa Mataifa, kama ilivyo kwa Somaliland.
Kujiunga na Umoja wa Mataifa
Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Kifungu cha 4 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, nchi inayotafuta uanachama katika Umoja wa Mataifa lazima ipate kura tisa kutoka wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na haipaswi kupingwa na nchi tano zenye kura ya turufu.
Mambo mengine yaliyotajwa katika mkataba huo ni pamoja na; nchi inayojiunga na Umoja wa Mataifa lazima ipate uungwaji mkono wa theluthi mbili ya nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ikiwa na maana kwamba nchi 129 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ziunge mkono.
Serikali ya Somalia imechukua hatua kadhaa kutafuta usaidizi wa kimataifa tangu uamuzi wa Israel utangazwe.
Umoja wa Afrika, IGAD, Umoja wa nchi za Kiarabu, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, na serikali kadhaa ikiwa ni pamoja na Misri, Uturuki, Saudi Arabia, Jordan, Qatar, Kuwait, na nchi zingine zimetoa taarifa zinazounga mkono uhuru wa Somalia.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura kuhusu Israel kuitambua Somaliland.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi