Machafuko kwenye maeneo ya magharibi na kusini mwa Sudan yamesababisha watu zaidi ya elfu 10 kukimbia makazi yao katika muda wa siku tatu ndani ya wiki moja, hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la wahamiaji, IOM.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Tangu mwezi April mwaka 2023, jeshi la serikali na wapiganaji wa RSF wamekuwa wakipigana katika kile Umoja wa Mataifa umekiita ‘vita ya kikatili’ ambayo hadi sasa imesababisha vifo vya maelfu ya raia huku wengine zaidi ya milioni 11 wakigeuka kuwa wakimbizi kwenye nchi yao.

Kwa mujibu wa IOM, kati ya Desemba 25 na 26, mashambulio kwenye vijiji vya Baru na Kernoi vinavyopakana na Chad, yalisababisha watu zaidi ya elfu 7 kukimbia makazi yao.

Baada ya kuuchukua Mji wa kaskazini mwa Darfur wa El fasher mwezi Oktoba, wapiganaji wa RSF walielekeza mashambulio yao upande wa magharibi ambako jamii za Zaghawa na wapiganaji wengine wanaoshirikiana na jeshi la Serikali wanaudhibiti.

Aidha IOM kwenye taarifa yake imeongeza kuwa usiku wa kuamkia Krismas hadi siku ya Ijumaa watu wengine zaidi ya Elfu 3 walikimbia toka kwenye Mji wa Kadugli ulioko Korodofan Kusini, Mji ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na njaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *