DC Ilala aagiza waliomuua Salehe wakamatweDC Ilala aagiza waliomuua Salehe wakamatwe

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Yustino Mgonja kutumia utaalamu na timu yake kukamata mara moja kundi la watu waliofanya mauaji ya Mzee Salehe Idd Salehe.

Salehe ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Zavala, Kata ya Buyuni wilaya ya Ilala Dar es salaam alivamiwa akiwa nyumbani kwake na kundi la wahalifu Desemba 4, 2025 saa 11:00 alfajiri na alifariki siku hiyo akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Amana.

Mpogolo alitoa agizo hilo wiki iliyopita kwenye mkutano wake na wananchi uliofanyika katika Mtaa wa Zavala baada ya kupata taarifa za uvamizi wa kinyama aliyofanyiwa mzee huyo akiwa nyumbani kwake na baadaye kusababisha kifo chake. SOMA: Serikali kutatua mgogoro wa ardhi ngara

Akizungumza katika mkutano huo Mpogolo amesema mzee Salehe katika maisha yake amekuwa mzalendo wa kweli kwa kupigania maeneo ya wazi ya serikali mfano shule, masoko na vituo vya afya yasichukuliwe na genge la wahalifu wanaouza maeneo hayo ya viwanja vilivyopimwa na serikali katika Programu ya Viwanja 20,000 Kata ya Buyuni kati ya miaka ya 2003/2005.

“Kamanda RPC wa Ilala nakuagiza tumia vyombo vyako na utaalamu wako na ninahakika unaweza kuakikisha mnawakamata watu wote waliofanya mauaji haya na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Kwa kuwa wauaji hawa inaelekea wanao mtandao mkubwa wa kiuhalifu katika eneo letu la Wilaya za kipolisi za Chanika na Ukonga,” alisema Mpogolo.

Wakatihuohuo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji kupitia Idara ya Mipango Jiji kuendelea kuyatambua na kuyarejesha maeneo yote ya wazi ya huduma za jamii yaliyolipiwa na kutengwa na serikali. Pia washirikiane na Jeshi la Polisi kubaini genge la wahalifu wa viwanja vya umma wanaouza kwa watu wasiojulikana.

Awali, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Zavala, Faridu Rashidi amesema katika Mtaa wa Zavala Kata ya Buyuni kwa sasa wananchi wanakaa kwa hofu kubwa kwa kuhofia kundi la watu wasiojulikana ambao wamefanya mauaji hayo. Rashid amesema kwa sasa wananchi wanaogopa kuongea kutokana na vitendo hivyo na wengine wamekimbia makazi yao hasa wale waliokuwa wanatetea maeneo ya huduma za jamii yasiuzwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *