Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa zaidi ya watu 10,000 wamelazimika kuhama makazi yao katika siku tatu katika majimbo ya Darfur Kaskazini na Kordofan Kusini mwa Sudan, huku vita vikiendelea nchini humo kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa RSF.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) la Umoja wa Mataifa liliripoti jana Jumapili kwamba zaidi ya watu 7,000 wamekimbia miji ya Um Buru na Karnoi huko Darfur Kaskazini, ambayo ilitekwa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) siku chache zilizopita.

Shirika hilo pia limeripoti kwamba zaidi ya watu 3,000 wamekimbia mji wa Kadugli huko Kordofan Kusini, ambao umezingirwa na wapiganaji wa RSF, huku watu wake wakiendelea kuteseka kwa njaa.

Pia huko Kordofan Kusini, moto umeteketeza makazi 45 ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo la Abu Jubaiha.

Katika taarifa tofauti, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwamba idadi ya watu waliokimbia makazi yao inaongezeka kwa kasi katika majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa Kordofan kutokana na “kuongezeka kwa ukosefu wa usalama”.

Mapigano kati ya jeshi la taifa la Sudan na wanamgambo wa RSF yameongezeka katika miji ya Kordofan katika miezi ya hivi karibuni tangu wapiganaji wa RSF walipoimarisha uwepo wao katika eneo lote jirani la Darfur, na kudhibiti mji wa El Fasher mwezi Oktoba mwaka huu.

Hali hiyo imezidisha Mateso ya watu nchini Sudan katika vita vilivyozuka Aprili 2023 kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Hadi sasa makumi ya maelfu na watu wameuawa na wengine milioni 13 wamekimbia makazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *