Kanali mmoja mstaafu wa jeshi la Saudia ametoa kauli kali ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) akisema kuwa, nchi hiyo ni mkono wa utawala wa Kizayuni unaofanya kazi ya kuzidhoofisha na kuziangamiza nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia.

Shirika la Habari la Tasnim limeweka mkanda wa video ambao ndani yake, Kanali Jassem Abu Abdul Rahman wa Saudi Arabia analaani na kulalamikia vitendo vya Imarati vya kutaka kuigawa vipande vipande Saudia na kushiriki kwake kwenye jinai huko nchini Sudan akisema: “Imarati ni mkono wa Israel wa kuzidhoofisha na kuziangamiza nchi za ukanda huu, na hili liko wazi sana katika baadhi ya nchi, kwamba lengo kuu au la kimkakati la Imarati ni kuiangamiza na kuidhoofisha Saudia.

Amesema: “Imarati hivi sasa inacheza mchezo mchafu na wa siri sana wa vyombo vya habari. Kuingilia kwake kijeshi Sudan kuko wazi kabisa na hawawezi tena kukataa.”

Ameongeza kwa kusema: “Bunge la Marekani limezungumza kuhusu suala hilo na kutoa mwito wa vikwazo dhidi ya Imarati… Hawawezi tena kusema kwamba hatuna jukumu lolote katika matukio ya Sudan.”

“Si kwamba tunasema tu maneno yasiyo na ushahidi, hapana, Marekani yenyewe imesema kwamba Rubio (Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani) alipokwenda Imarati aliwaomba waache kuunga mkono Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF),” amesema.

Inalalamikiwa duniani kwamba kundi la RSF huko Sudan ni la wanamgambo wa mamluki wanaoungwa mkono na Imarati na wanaendesha mashambulizi yao kwa silaha za Marekani kwa sababu Imarati inawapa silaha zilizotengenezwa Marekani.

Matamshi ya kanali huyo wa kijeshi wa Saudia ni ushahidi wa kuzidi kuharibika uhusiano baina ya Riyadh na Abu Dhabi kiasi kwamba afisa huyo wa kijeshi wa Saudia ametoka hadharani na kulalamika kwamba Imarati inafanya njama za kuigawa vipande vipande Saudi Arabia na kwamba ni mkono wa Israel wa kuzivuruga ndhi za ukanda huu hasa Saudia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *