Uingereza imeibua wimbi kubwa la mijibizo na malalamiko ya ndani na ya kimataifa kwa hatua yake ya kuweka vizuizi vya viza na kupitisha mageuzi makali kwa utoaji hifadhi ya ukimbizi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ilitangaza Jumamosi kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC imepokonywa fursa ya upendeleo wa viza kwa kutotoa ushirikiano katika suala la kuwarudisha nchini humo wahamiaji wasio na vibali na wahalifu wa kigeni. Kwa sababu hiyo, DRC haitaweza kupata huduma za viza za haraka na za upendeleo kwa ajili ya maafisa wake muhimu.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Shabana Mahmood ameonya kwamba, ikiwa serikali ya Kongo itaendeleza mwenendo wa kutotoa ushirikiano, utoaji viza kwa nchi hiyo utasimamishwa kikamilifu.

Tunatarajia nchi zichukue hatua kwa mujibu wa sheria. Ikiwa mmoja wa raia wao hana haki ya kuwepo hapa, lazima wamrejeshe,” ameeleza waziri huyo.

Shabana Mahmood (kulia)

Kwa mujibu wa ripoti, katika miezi ya karibuni Kongo, DR imekataa kuwapokea mamia ya wahamiaji haramu na hata wahalifu hatari, wakiwemo wa utumiaji nguvu na wa ukatili wa kingono. Hatua hiyo imetafsiriwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza kama “ukwamishaji wa moja kwa moja.” Kwa upande mwingine, na baada ya kuandamwa na vitisho sawa na vilivyotolewa dhidi ya DRC, Angola na Namibia zimeripotiwa kuwa zimezidi kutoa ushirikiano na kukubali kuwarudisha nyumbani raia wao.

Sera hiyo mpya ya serikali ya Uingereza imekabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mshauri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mark Davis, ameiita kitu cha “kuaibisha” na kilicho kinyume na ahadi ya kihistoria iliyojifunga nayo Uingereza kwa wakimbizi. Kiongozi wa zamani wa chama cha Leba, Jeremy Corbyn, yeye ameitaja sera hiyo kuwa ni “ukatili” na akasema uamuzi wa serikali umelenga “kuwaridhisha wafuasi wa mrengo wa kulia”. Anwar Suleiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Wakimbizi ametahadharisha kuwa, mipango hiyo haitawazuia kuvuka na kuingia Uingereza watu wanaotafuta hifadhi; na kwamba wale wanaojipinda na kuchapa kazi inapasa wawe na uwezo wa kujenga “maisha salama na ya utulivu”.

Hatua hizo zinazoshuhudiwa ni sehemu ya mpango wa mageuzi makubwa ulioanzishwa mwezi uliopita na serikali ya Waziri Mkuu Keir Starmer. Kwa mujibu wa mageuzi hayo, hali ya ukimbizi itafanywa kuwa ya muda na kupitiwa upya kila baada ya miezi 30. Wakimbizi watalazimika kurudi katika nchi zao mara tu itakapobainika kuwa ziko salama na watapaswa kusubiri kwa miaka 20 kwa ajili ya kupata makazi ya kudumu, muda ambao ni mrefu mara nne zaidi ya wa hivi sasa.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza ameuita mfumo unaotumika hivi sasa kuwa “usiodhibitiwa na usio wa haki” na akasema, lengo la mageuzi hayo ni kuwazuia wanaotafuta hifadhi wasivuke Mkondo wa maji wa Uingereza kwa kutumia boti ndogo.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, zaidi ya watu 39,000 wamewasili nchini Uingereza mwaka huu kwa usafiri wa boti ndogo; idadi ambayo ni kubwa zaidi kulinganisha na mwaka mzima wa 2024, japokuwa ni ndogo zaidi ikifananishwa na ya mwaka 2022. Maombi ya kupatiwa hifadhi yameongezeka pia katika kipindi cha hadi Juni 2025 kwa kufikia watu laki moja na elfu 11, kikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa. Kwa upande mwingine, uhamiaji halisi umepungua kutoka rekodi ya watu 906,000 katika mwaka 2023 hadi 431,000 mwaka 2024, ikiwa ni ishara ya athari za sheria kali zaidi zilizowekwa.

Wahamiaji wanaoomba hifadhi Uingereza

Waziri wa Mambo ya Nje Yvette Cooper ametangaza kuwa, tangu mwezi Julai mwaka huu, zaidi ya watu 50,000 ambao hawakuwa na haki ya kuishi nchini Uingereza wamefukuzwa, likiwa ni ongezeko la 23% ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

Vizuizi vipya vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mageuzi makubwa yaliyofanywa katika utoaji hifadhi yameiweka Uingereza katika hali nyeti na hasasi. Kwa upande mmoja, serikali inajaribu kuimarisha udhibiti wa mipaka na kuziwekea mashinikizo nchi inazoziita “wakwmaishaji”; na kwa upande mwingine, inakabiliwa na ukosoaji wa ndani na wa kimataifa kwa kukiuka haki za binadamu. Mustakabali wa sera hizi utategemea kiwango cha ushirikiano zitakaotoa nchi zinazolengwa na uwezo wa serikali ya London wa kuweka mlingano kati ya usalama na wajibu wa kiutu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *