
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kwamba uwepo wowote wa Israel huko Somaliland utatambuliwa kama shabaha ya kijeshi, kwa sababu ni uchokozi dhidi ya Somalia na Yemen na tishio la moja kwa moja kwa usalama wa kikanda ambalo lazima likabiliwe kwa hatua madhubuti.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili, Abdul-Malik al-Houthi alilaani vikali hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland kama taifa huru na kusema: “Ni hatua ya kikatili ya Kizayuni” yenye lengo la kuanzisha msingi wa kuwepo katika Pembe ya Afrika.
Al Houthi amesema kwamba uwepo wowote wa Israel huko Somaliland ni “tishio la moja kwa moja” kwa usalama wa kikanda, haswa Bahari Nyekundu na njia za meli za Ghuba ya Aden.
Amesema kwamba Israel inataka kuzigawanya nchi za eneo hilo kama sehemu ya mpango mpana wa kuunda upya eneo la Asia Magharibi.
“Hatua hii ya Wazayuni, ambayo inalenga kupata sehemu ya kuweka guu nchini Somalia ili kuzigawa nchi za eneo hilo katika mpango ambao hauishii Somalia, ambao jina lake lililotangazwa ni kubadilisha Mashariki ya Kati, ni jambo ambalo taifa letu linapaswa kukabiliana nalo kwa nguvu zote,” amesema Abdul-Malik al-Houthi.
Amepuuza mbali hatua ya Israel ya kutambua rasmi eti nchi huru ya Somaliland akiitaja kuwa “haina thamani yoyote katika mizani ya sheria.”
Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ametoa wito kwa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuiunga mkono mamlaka ya kujitawala ya Somalia, akihimiza kuzidisha mashinikizo kwa washirika huko Somaliland na kuchukua misimamo imara katika taasisi za kimataifa.