
Jeshi la Israel limewaua watu 706 kutoka familia za waandishi wa habari katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari mnamo Oktoba 7, 2023. Taarifa hii ni kwa kujibu wa ufuatiliaji na nyaraka za Muungano wa Waandishi wa Habari wa Palestina.
Muungano huo umetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru wa kimataifa, na kuchukuliwa hatua za ndani za Kiarabu na kimataifa, ili kuwalinda waandishi wa habari wa Palestina na familia zao, na kujumuishwa mashambulizi ya Israel dhidi ya familia za waandishi wa habari katika faili za mashtaka yanayowasilishwa kwenye mahakama za kimataifa.
Ripoti ya Kamati ya Uhuru ya Muungano wa Waandishi wa Habari wa Palestina imefichua kwamba mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari wa Palestina hayakuishia katika mauaji ya moja kwa moja, kujeruhi, kuwakamata au kuzuia shughuli za upashaji habari, bali yamechukua mkondo hatari na wa kikatili zaidi ikiwa ni pamoja na kulenga familia za waandishi wa habari na jamaa zao, katika juhudi zisizokoma za Israel za kugeuza kazi ya uandishi wa habari kuwa jinai ambayo gharama yake inalipwa na watoto, wake, baba na mama wa waandishi wa habari.
Hadi sasa, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali huko Gaza imerekodi mauaji ya waandishi wa habari 257, kutokana na kulengwa moja kwa moja na askari wa Israel kwa lengo la kukandamiza upashaji habari na kunyamazisha simulizi ya Palestina.
Muungano wa Waandishi wa Habari wa Palestina umeeleza kwamba kulenga familia za waandishi wa habari kumekuwa utaratibu wa kimfumo unaokaririwa katika miaka ya 2023, 2024 na 2025, na kusema kwamba viashiria vyote vinathibitisha kwamba mashambulizi hayo hayakuwa matukio ya bahati mbaya yaliyotokana na vita.
Taarifa ya muungano huo imesema kuwa tukio la hivi karibuni ni lile la siku chache zilizopita, wakati mwili wa mwandishi wa habari, Hiba al-Abadla, mama yake na takriban watu 15 wa familia ya al-Astal ilipopatikana, karibu miaka miwili baada ya shambulio la Israel dhidi ya nyumba yao, magharibi mwa Khan Yunis.
Takwimu zinaonyesha kwamba mamia ya watoto, wanawake na wazee wameuawa kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza kwa sababu tu ya taaluma ya mwanafamilia na uandishi wa habari, huku ushahidi ukionyesha kwamba mashambulizi hayo yalichukua sura mbalimbali, hasa mabomu ya moja kwa moja kwenye nyumba za waandishi wa habari, ambayo yalisababisha vifo vya idadi kubwa ya wanafamilia wao, na katika baadhi ya matukio kuuawa kwa familia nzima.