Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi amesema kuna ulazima wa kulindwa umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Yemen, huku kukiwa na ongezeko la mvutano katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Araqchi ametoa kauli hiyo katika mazungumzo tofauti ya simu, jana Jumapili, na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, Faisal bin Farhan Al Saud na Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemwambia mwenzake wa Saudi Arabia kwamba ramani ya kisiasa, inayopendekeza kusitisha mapigano na kupatikana suluhisho pana zaidi kwa njia ya mazungumzo katika miezi ijayo, lazima itekelezwe.

Machafuko ya sasa nchini Yemen yalishadidi zaidi tarehe 3 Desemba huku vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini (STC) vinavyosaidiwa na UAE vikinyakua udhibiti wa Hadramout baada ya mapigano makali na wanamgambo wanaoungwa mkono na Saudi Arabia.

Baada ya unyakuzi huo wa STC, Saudi Arabia ilifanya mashambulizi ya anga Ijumaa iliyopita, ikilenga maeneo ya STC. 

Sayyid Abbas Araqchi pia amelaani uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon na kusema, jamii ya kimataifa na wadhamini wa makubaliano ya kusitisha mapigano wanabeba jukumu la kusimamisha mashambulizi na uhalifu wa utawala huo dhidi ya watu wa Lebanon.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, amesisitiza umuhimu wa kuendelewa mashauriano na ushirikiano miongoni mwa nchi za kikanda ili kulinda amani na utulivu.

Faisal bin Farhan Al Saud amesema utawala wa Israel lazima uwajibishwe kwa ukatili wake katika eneo la Asia Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *