
Rabat, Morocco. Cameroon na mabingwa watetezi Côte d’Ivoire usiku wa kuamkia leo walitoshana nguvu kwa sare ya 1–1 katika mchezo wa pili wa Kundi F wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, uliochezwa Marrakech. Baada ya dakika 90 zenye ushindani mkubwa, hakuna timu iliyoweza kupata ushindi.
Junior Tchamadeu alifunga bao la kusawazisha katika kipindi cha pili baada ya shuti lake kumgonga beki Ghislain Konan, na kufuta bao la awali la kuvutia lililofungwa na Amad Diallo kwa Côte d’Ivoire.
Mchezo ulianza kwa tahadhari kubwa kutoka pande zote. Cameroon ilikaribia kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 20 kupitia Christian Kofane, lakini kichwa chake kiligonga mwamba wa lango.
Côte d’Ivoire walidhani wamepata bao kabla ya mapumziko baada ya Franck Kessié kufunga, lakini bao hilo lilikataliwa kwa sababu ya kuotea.
Kipindi cha pili kilikuwa cha kasi kubwa. Diallo alifunga bao la kwanza kwa shuti la kali lililomshinda kipa Devis Epassy. Hata hivyo, Cameroon walirejea haraka dakika tano baadaye kupitia Tchamadeu.
Licha ya mashambulizi kutoka pande zote hadi mwisho wa mchezo, hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao la ushindi. Sare hiyo inaacha Cameroon na Côte d’Ivoire zikiwa na pointi nne kila moja zikiwa na nafasi ya kufuzu.
Cameroon watacheza na Msumbiji katika mchezo wa mwisho wa kundi, huku Côte d’Ivoire wakibaki Marrakech kuivaa Gabon ambayo haina matumaini.
Algeria 1–0 Burkina Faso
Bao: Riyad Mahrez (pen) 23’
Nahodha Riyad Mahrez alifunga bao pekee la penalti lililoihakikishia Algeria ushindi na tiketi ya kufuzu hatua ya 16 bora AFCON 2025.
Algeria sasa wana pointi sita kileleni mwa Kundi E baada ya kushinda michezo miwili mfululizo. Burkina Faso wanabaki nafasi ya pili na pointi tatu, sawa na Sudan.
Mchezo ulikuwa wa nguvu na mapambano makali. Algeria walipata pigo mapema baada ya Juan Hadjam kuumia na kutolewa nje dakika ya 13.
Dakika ya 23, Rayan Aït-Nouri alifanyiwa madhambi ndani ya boksi, na Mahrez akafunga penalti kwa utulivu.
Algeria walitawala pia kipindi cha pili lakini wakashindwa kuongeza mabao. Burkina Faso walijaribu kusawazisha bila mafanikio.
Algeria sasa watacheza na Equatorial Guinea, huku Burkina Faso wakipambana na Sudan katika mchezo wa kuamua nani atafuzu.
Equatorial Guinea 0–1 Sudan
Bao: Saúl Coco (kujifunga) 74’
Sudan walipata ushindi muhimu wa bao 1–0 dhidi ya Equatorial Guinea katika hali ya baridi kali ya nyuzi 14 jijini Casablanca.
Bao pekee la mchezo lilitokana na kujifunga kwa beki Saúl Coco baada ya jaribio la kuokoa krosi ya Sudan.
Ushindi huu ni wa kwanza kwa Sudan katika fainali za AFCON tangu mwaka 2012, na umefanya Kundi E kuwa wazi zaidi.
Kipa Monged Abuzaid alikuwa nguzo muhimu kwa Sudan, akiokoa mashambulizi mengi ya Equatorial Guinea.
Sudan sasa wanakwenda katika mchezo wa mwisho dhidi ya Burkina Faso wakiwa na matumaini makubwa ya kufuzu hatua ya mtoano.
Gabon 2–3 Msumbiji
Wafungaji:
Gabon: Aubameyang 45+5, Moussounda 86
Msumbiji: Bangal 37, Catamo (P) 42, Calila 52
Msumbiji waliandika historia kwa kupata ushindi wao wa kwanza kabisa katika fainali za AFCON baada ya kuifunga Gabon 3–2.
Faizal Bangal alifungua ukurasa wa mabao, kabla ya Geny Catamo kufunga penalti. Gabon walipata bao kabla ya mapumziko kupitia Pierre-Emerick Aubameyang.
Kipindi cha pili, Diogo Calila aliiongezea Msumbiji bao la tatu. Gabon walijaribu kurejea mchezoni na kufunga bao la pili, lakini walishindwa kusawazisha.
Kipa Ernan Siluane alifanya kazi kubwa kuilinda Msumbiji hadi filimbi ya mwisho.
Ushindi huu umehitimisha takribani miaka 40 ya kusubiri kwa Msumbiji kupata ushindi katika AFCON.