Safari ya kulisaka taji la Mapinduzi 2026 ilianza jana Jumapili, Desemba 28, 2025 kwa kupigwa mechi moja ya kundi A tofauti na mwanzo ilivyopangwa zitachezwa mbili. Mlandege ilipambana na Singida Black kisha, huku Azam dhidi ya URA ikisogezwa mbele.

Kuanza kwa michuano hiyo kunafungua mlango mwingine wa kumsaka bingwa baada ya mara ya mwisho kufanyika mwaka 2024 ikishirikisha timu za klabu, Mlandege kuwa mabingwa.

Mlandege kutoka Unguja, imefungua dimba ikilisaka taji la tatu la michuano hiyo baada ya kuchukua mfululizo mwaka 2023 ikiifunga Singida Big Stars fainali na 2024 ikiichapa Simba.

Wakati michuano hiyo ikianza jana Desemba 28, 2025, kilele chake ni Januari 13, 2026. Hapa kuna mambo kadhaa yanayosubiriwa katika michuano hiyo itakayodumu kwa takribani siku 17 huku wanaume kutoka timu kumi wakitoana jasho. Humo ndani watu wanasaka rekodi, mkanjwa kwa washindi, lakini pia burudani kwa mashabiki.

Kabla ya kwenda mbali, timu kumi shiriki ni Azam, Simba, Yanga, Singida Black Stars na TRA United kutoka Tanzania Bara.

Pia zipo Mlandege, Mwembe Makumbi na KVZ za Unguja na Fufuni kutoka Pemba, huku URA ikitokea Uganda.

Msako wa milioni 150

Tofauti na ilivyokuwa awali bingwa anakabidhiwa Sh100 milioni huku nafasi ya pili akilamba Sh70 milioni, safari hii mzigo umeongezwa.

Mzigo wa bingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026 ni Sh150 milioni huku nafasi ya pili akibeba Sh100 milioni.

Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman, anasema: “Thamani ya Kombe la Mapinduzi ni kubwa, hiyo ndio sababu ya kuongeza fedha kwani mwenye mapinduzi yake, Rais Mwinyi ameona hilo ni jam[1]bo muhimu kuipa heshima michuano hii kwa kuanzia mwaka huu.

“Lakini pia wadhamini wameipa thamani kubwa Mapinduzi Cup ya safari hii, tunawashukuru sana kwa mchango wao kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.”

Mzuka Unguja hadi Pemba

Safari hii kipute kinapigw Unguja na Pemba tofauti na mwanzo ikifanyika eneo moja mwanzo hadi mwisho.

Mara ya mwisho michuano iliyopita ziliposhiriki timu za taifa, ilichezwa kisiwani Pemba kwenye Dimba la Gombani, kabla ya hapo ilifanyika New Amaan Complex kisiwani Unguja.

Katibu Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman, anasema: “Fainali kama kawaida imekuwa ikichezwa Januari 13 kila mwaka na safari hii itafanyika Pemba kwenye Uwanja wa Gombani.

“Tunamshukuru Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi kwa kuufanyia maboresho Uwanja wa Gombani ambao umekuwa wa kisasa zaidi kama alivyofanya Uwanja wa New Amaan Complex ambao leo hii mechi kubwa za kimataifa zinachezwa hapa Zanzibar.”

Wenyeji kazi ipo

Mashindano hayo yalipoanza kufanyika mwaka 2007 katika mfumo wa sasa ukihusisha timu za Zanzibar na nje ya visiwani humo, Yanga ilikuwa ya kwanza kutwaa ubingwa, ikarudia tena mwaka 2021, msimu huu ina nafasi ya kutanua wigo wake wa ubingwa kufukuzia rekodi ya Simba iliyobeba mara nne (2008, 2011, 2015 na 2022) na Azam ikiongoza kwa kuchukua mara tano (2012, 2013, 2017, 2018 na 2019).

Timu zingine zilizobeba ubingwa wa mashindano hayo ni Mlandege (2023-2024), Mtibwa Sugar (2010 na 2020), Miembeni (2009), KCCA (2014), URA (2016) na Zanzibar Heroes (2025).

Ukiangalia orodha ya mabingwa, inabaki kuwa mtego kwa wenyeji kupambana kulibakisha kombe kama ilivyokuwa 2023 na 2024 kwani kabla ya hapo, mara ya mwisho timu ya Zanzibar kushinda Kombe la Mapinduzi ilikuwa mwaka 2009, likibebwa na Miembeni.

Zanzibar ilisubiri takribani miaka 14 kulibakisha taji visiwani kutoka 2009 hadi 2023, baada ya hapo imefanikiwa mara tatu mfululizo.

Ukiiweka kando Mlandege iliyochukua 2023 na 2024, Zanzibar Heroes imekuja kubeba 2025 michuano iliposhirikisha timu za taifa.

Mbali na Miembeni, Mlandege na Zanzibar Heroes, taji hilo limevuka maji mara kadhaa kwa kutua Dar, Morogoro na kuvuka boda likienda Uganda mara mbili. Mwaka 2014 likichukuliwa na KCCA, kisha 2016 ikawa zamu ya URA.

Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohamed ‘Man Gamera’ anasema hadi sasa hajakiona kitu cha kumshtua kwa wapinzani wake isipokuwa Simba kwa sababu ina uzoefu wa mashindano makubwa na kuwa na wachezaji wa kimataifa.

Anasema, hata hivyo mpira wa miguu ni mchezo wa wazi na kitu ambacho anapaswa kukizungumzia kwasasa ni udogo wa timu hiyo kushiriki mashindano hayo licha ya kwamba sio sababu ya kushindwa kwani wamejiandaa vizuri.

“Fufuni bado ni timu ndogo ambayo haina uzoefu hata kwenye ligi Kuu Zanzibar, lakini imeonesha ushindani wa hali ya juu kwa kuwafunga magwiji, hivyo hata huku tutawaonyesha,” anasema.

Kocha huyo ameongeza kwmaba, lengo lake ni kuiona timu hiyo ikifika fainali na kuchukua kombe kwenye ardhi ya nyumbani kisiwani Pemba, huku akiwa na imani kubwa ya kufanya vizuri.

Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China anasema timu hiyo imejipanga kutetea ubingwa wake na hawawezi kuruhusu kuchukuliwa na timu nyingine.

Naye, Ofisa Habari wa KVZ, Aljalil Mohamed anasema ujio Kocha Mkuu, Malale Hamsini ni miongoni mwa maboresho ya kikosi hicho katika kujiandaa kufanya vizuri kwenye Mapinduzi Cup 2026.

Anasema, kama walifanikiwa kuvuka hatua ya robo fainali awali, mwaka huu lengo lao ni kufika fainali ambayo itachezwa kisiwani Pemba.

Anaeeleza kuwa, sababu ya kumchukua Malale kwenye benchi hilo la ufundi wanaona anaweza kuivusha timu hiyo ikiwa salama kutokana na uzoefu wake.

Ofisa Habari wa Mwembe Makumbi,  Hemed Suleiman ‘London Boy’ anasema timu hiyo itahakikisha inatoboa kwenye kundi ililipo, haijalishi imepangwa na nani.

Anasema, katika kuona hilo linafanikiwa, wamefanya maboresho maeneo kadhaa ikiwemo eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa pasua kichwa upande wao ambapo imemrudisha visiwani Idd Pina ambaye mwaka 2024 alichangia kuipa Mlandege ubingwa wa Mapinduzi, kabla ya kutimkia Pamba Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Bara akidumu kwa takribani miezi sita msimu huu 2025-2026.

Azam katika utawala wake

Kati ya timu kumi zinazoshiriki Kombe la Mapinduzi 2026, Azam ndio imelibeba mara nyingi ambazo ni tano, ikifuatiwa na Simba mara nne.

Kwa mwaka huu, Azam inataka kutanua wigo wa ushindi huku Simba ikiifukuzia kwa ukaribu sana.

Mbali na hilo, Azam kwa kuonyesha wao ni manguli, wamewahi kulitetea taji hilo mara mbili. Pia ndio timu pekee iliyobeba mara tatu mfululizo katika mwaka 2017, 2018 na 2019.

Kabla ya hapo, ilikuwa timu ya kwanza na pekee kubeba mara mbili mfululizo, 2012 na 2013, Mlandege ikaja kulipa 2023 na 2024.

Tayari Kocha wa Azam, Florent Ibenge amepiga mkwara akisema: “Azam ni timu kubwa, hakuna shindano tunakwenda bila malengo ya ku[1]chukua ubingwa.”

Yanga, Simba kujiuliza

Wakongwe wa soka la Bongo, Yanga na Simba ni kama hawana upepo mzuri katika Kombe la Mapinduzi.

Kidogo Simba imeonyesha umwamba kwa kubeba mara nne, lakini Yanga imechukua mara mbili pekee.

Mara ya mwisho Simba ilibeba ubingwa mwaka 2022, kabla ya hapo, Yanga ilichukua 2021.

Timu hizo zimekuwa zikikaa muda mrefu bila ya kubeba kombe hilo hali inayowanyima mzuka mashabiki wao.

Yanga ikiwa imechukua 2007 na 2021, kuna gepu la miaka 14 kutoka taji la kwanza hadi la pili. Kwa upande wa Simba, ilikuwa 2008, 2011, 2015 na 2022.

Kutoka taji moja kwenda lingine, ilipita miaka mitatu, ikafuatia miaka minne, kisha saba.

Timu hizo hazijawahi kutetea ubingwa, ni Azam na Mlandege pekee zimetetea taji la michuano hiyo.

Ni muda wa Simba na Yanga kujiuliza huku zikishiriki zikiwa na mabenchi mapya ya ufundi. Simba inaye Steve Parker na Yanga yupo Pedro Goncalves.

ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI

2007       Yanga

2008       Simba

2009       Miembeni

2010       Mtibwa Sugar

2011       Simba

2012       Azam

2013       Azam

2014       KCCA

2015       Simba

2016       URA

2017       Azam

2018       Azam

2019       Azam

2020       Mtibwa Sugar

2021       Yanga

2022       Simba

2023       Mlandege

2024       Mlandege

2025       Zanzibar Heroes

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *