Syria Observatory yenye makazi yake nchini Uingereza, imenukuu mtandao wake wa wanaharakati ndani ya Syria na kusema maandamano hayo yalizuka katika mikoa kadhaa, ikiwa ni pamoja na Latakia, ambao ni makazi ya idadi kubwa ya jamii ya wachache ya Alawi .
Pia imesema maandamano kama hayo yaliripotiwa katika mikoa ya Tartus, Homs na Hama.
Makumi ya waandamanaji wajeruhiwa
Picha zilizochapishwa na shirika la habari la serikali SANA, zilionyesha vikosi vya usalama, pamoja na magari ya kivita, yakipelekwa katika mzunguko wa al-Azhari huko Latakia, kitovu cha maandamano hayo ya kuipinga serikali.
Makumi ya waandamanaji walijeruhiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na visu.
Hata hivyo SANA imeripoti kuwa mamlaka ya Syria, imewalaumu wafuasi wa rais wa nchi hiyo aliyepinduliwa Bashar al-Assad kwa kushambulia vikosi vya usalama na raia wakati wa machafuko ya Latakia na kusababisha vifo hivyo vya watu watatu.
Pia imenukuu mamlaka ya afya ikisema kuwa takriban watu wengine 60 walijeruhiwa Latakia.
Wakati huo huo, wizara ya mambo ya ndani imesema afisa mmoja wa vikosi vya usalama aliuawa na wengine kujeruhiwa walipokuwa wakidhibiti maandamano hayo ya Latakia. Haikubainika mara moja ikiwa kifo hicho ni miongoni mwa vifo hivyo vitatu vilivyoripotiwa na mamlaka ya afya.
Mmoja wa waandamanaji wanaoiunga mkono serikali Mohammad Bakkour, alisema walikuwa hapo kuiunga mkono serikali yao mpya ambayo tangu siku ya kwanza ya kile alichokitaja kuwa ukombozi ilitoa wito wa amani na kutoa msamaha kwa wahalifu.
”Hata hivyo wahalifu hao hawakukubali msamaha huo na wanaendelea kuleta matatizo ili kuhujumu fursa mpya ya kulijenga taifa. Watu wote wanataka umoja na nchi moja, lakini wao hawataki umoja na nchi moja, wanataka mgawanyiko wa kidini, machafuko na matatizo kwa maslahi yao binafsi.”
Serikali yalaani kutokea kwa mashambulizi
Kupitia taarifa katika mtandao wa Telegram, kundi moja lisilo maarufu linalojiita Saraya Ansar al-Sunna lilidai kuhusika katika shambulizi hilo la Ijumaa na kusema lililenga wanachama wa jamii ya Alawi ambayo Waislam wenye misimamo mikali wanawaona kuwa waasi.
Serikali ya Syria imelaani shambulizi hilo na kuahidi kuwawajibisha waliohusika ingawa bado haijatangaza kukamatwa kwa yeyote.