
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema kuwa upungufu wa maji uliotokea nchini haujasababishwa na uzembe, bali ni matokeo ya hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia kwa ujumla, ikiwemo Tanzania.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Desemba 29, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya maji katika Mto Ruvu.
Kauli hiyo imekuja kufuatia maelezo ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliyebainisha kuwa ukame na kuchelewa kwa mvua vimesababisha kupungua kwa uzalishaji wa maji.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 534 za maji kwa siku, hata hivyo kutokana na hali ya ukame, uzalishaji huo umeshuka hadi chini ya lita milioni 300.
“Kilichofanyika ni kuhakikisha maji yanayozalishwa yanatumika kwa usawa,”amesema.
Kutokana na kauli hiyo, Dk Mwigulu amesema mambo ya mabadiliko ya tabianchi yanapoongeleka hayana ladha kutokana na kukinzana na shughuli zenye ladha wakati huo.
“Siku zingine huwa tukichukua hatua kama Serikali huwa hazipokelewi kwa ladha na Watanzania kwa ujumla na sio kwa Tanzania tu ni jambo la dunia,”amesema.
Akizungumzia shida ya maji, Dk Mwigulu amesema tatizo sio la Dar es Salaam, Morogoro na Pwani bali ni la nchi nzima.
Dk Mwigulu ametolea mfano maisha yake akisema, “kwa sisi tuliokulia vijijini ukiangalia hali ya mazingira tuliyokuta na sasa kuna mabadiliko makubwa, madhara ya mabadiliko hayo ni kama haya ambayo yanajitokeza,” amesema.
Amesema pamoja na hivyo Serikali haijalala, miaka mitatu iliyopita ilianza kutafuta majawabu ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Ametoa ujumbe kwa waliozoea kuelezea matatizo, wakijibanza nje ya nchi kuwa Serikali haijalala.
“Pamoja na kwamba Serikali ilikuwa na kazi kubwa ya kutekeleza mradi mkubwa ambao kwa mtu yeyote angeweza kuwa na sababu yeyote ya kutotekeleza mradi mwingine,” amesema.
Akizungumzia ombi la Aweso, la kutolewa kwa fedha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa Mradi wa Kidunda, Dk Mwigulu, amesema Serikali itafanya kikao na Wizara ya Fedha kuhakikisha mradi huo unapewa kipaumbele, kama ilivyokuwa kwa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere.
Dk Mwigulu amesema hadi sasa Mradi wa Kidunda tayari umepangiwa Sh10 bilioni, ambazo zimeshatumika, huku kiasi cha Sh236 bilioni kikihitajika ili kukamilisha utekelezaji wake.
Aidha, amesema mradi mwingine unaohitaji kuanza kutekelezwa ni Mradi wa Maji wa Rufiji, ambao utekelezaji wake ni takwa la Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030.
Akizungumzia miundombinu ya barabara, Dk Mwigulu amesema barabara ya Kibaha inayoanzia Shule ya Baobab tayari imepata fedha, na mkandarasi yupo katika eneo la mradi akiendelea na kazi.
Kuhusu changamoto za maji kwa ujumla, Dk Mwigulu amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo, na kama isingekuwa hatua zilizochukuliwa mapema, athari za mabadiliko ya tabianchi zingesababisha madhara makubwa zaidi.
Ameongeza kuwa jijini Dar es Salaam kuna maeneo mengi yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ambayo awali wakulima walikuwa wakipata maji ya kunywesha mifugo, lakini kwa sasa vyanzo hivyo vimekauka.