Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema kuchelewa kwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kumeibuka kutokana na kuanza mradi huo wakati matatizo mengine ya msingi yakiwa bado yanashughulikiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maji ya Machi 2022, ujenzi wa bwawa hilo ulitarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022 hadi 2025.

Hadi sasa, mradi huo wa Sh335.5 bilioni umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake, na ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji.

Akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la pamoja na kituo cha mabasi eneo la Bunju B, Dar es Salaam, Dk Mwigulu amefafanua sababu za ucheleweshaji wa mradi huo.

“Kwa nini haikwenda kwa kasi kubwa sana ni kwa sababu bwawa hili limejengwa sambamba na matatizo mengine makubwa zaidi yakishughulikiwa,” amesema.

Dk Mwigulu amekumbusha kuwa miaka mitatu iliyopita kulikuwa na mgawo mkali wa umeme, na baadhi ya wataalamu walipendekeza kukodiwa mitambo, lakini Rais Samia Suluhu Hassan alikataa, akisisitiza kwamba mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ukamilike.

Amesema kwa sasa hakuna mgawo wa umeme, na tatizo lolote linalohusiana na umeme linafanyiwa matengenezo mara moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zenye ziada ya umeme zaidi ya megawati 2,000.

Akizungumzia tatizo la maji, Dk Mwigulu amesema amepita kujionea hali halisi kwenye chanzo cha maji, na kwa sasa hali hiyo inaridhisha.

 “Tumesharejea kwenye hali ya kawaida kwa hiyo hakuna kisingizio. Nikiwa nimetoka huko nimejionea hali halisi na nikiri mbele ya umma huu kwamba kilichotokea sio uzembe na tungechukua hatua kali sana,” amesema.

Amesema kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya tabianchi ambayo husababisha mtawanyiko wa mvua usio na mpangilio.

“Mtawanyiko wa mvua usio na mpangilio unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi moja ya sifa zake ni kama hizi, inatokea katika mwaka mmoja ya eneo kuna mafuriko kama ilivyotokea mwaka jana mafuriko wilayani Hanang,” amesema.

Amesema Serikali chini ya Rais Samia haijalala na wala haijaacha kukadiria mambo ambayo hayajatokea kwamba yatatokea.

Moja ya jambo alilotaja tayari limekadiriwa ni Serikali kuanza kujenga Bwawa la Kidunda ambalo litahifadhi maji mililita bilioni 190 na ujenzi wake ni asilimia 40.

Dk Mwigulu amesema hayo anayaeleza kutokana na kwamba wamekuwepo mafundi wa kuelezea matatizo kuliko kutoa suluhisho.

“Wao wanaorodhesha tatizo hilo, leo Serikali imeshapata mkandarasi miaka miwili iliyopita na jawabu lake ni bwawa,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema, si maeneo yote yalikuwa yakipata maji ikiwemo Mabwepande na Bunju.

Amesema bili zitakazokuwa zikitolewa kwa wananchi ziwe halisia kwa sababu hawakupata maji wakati wote.

“Haiwezekani mwananchi hakupata maji siku zote halafu unakuja kumwambia alipe bili laki saba kama ana kiwanda nyumbani, haiwezekani.

“Nataka niwaambie mameneja wa Dawasa mimi ni kijana mkinizingua tunazinguana,” amesema.

Aweso amesema kutokana na hali ilivyo sasa Dawasa hawana kisingizio wananchi wapate maji safi na salama kwa kuwa  yapo katika mtambo wa Ruvu Juu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *