
Uganda itaanza kuwapokea wahamiaji wasiokuwa na sifa ya kuishi nchini Marekani, hatua ambayo inaendeleza sera ya rais Donald Trump kuwaondoa wahamiaji haramu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua hii ya Uganda imethibitishwa na Vincent Bagiire,Katibu wa kudumu kwenye Wizara ya Mambo ya nje, kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X, siku ya Ijumaa.
Bagiire, ameeleza kuwa Kampala imekubaliana na Marekani kuwapokea wahamiaji hao, wasio tayari kurejea katika nchi wanazotoka, mpango ambao hata hivyo amesema ni wa muda mfupi.
Hata hivyo, ameongeza kuwa, wahamiaji wenye rekodi ya uhalifu na watoto wasiokuwa na wazazi hawataruhusiwa kuja nchini Uganda inayowapa hifadhi wakimbizi zaidi ya Milioni 1.7.
Aidha, serikali ya Uganda imesema, itawapokea tu, wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika, wanaofukuzwa Marekani na kwa sasa nchi hizo mbili, zipo kwenye mazungumzo ya namna ya kutekeleza mpango huo.
Uganda sasa inajiunga na mataifa ya Rwanda, Sudan Kusini, Eswatini na El Salvador ambayo yameingia kwenye mkataba wa namna hii na Marekani chini ya rais Donald Trump, licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu.