Katika zama hizi za kidijitali, taasisi, mashirika na vyama vya wafanyakazi kote ulimwenguni vinaendelea kubadilisha njia za kufanya kazi ili kukidhi mahitaji ya wanachama, kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya kitaasisi na kijamii kwa kutumia teknolojia.
Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha Huduma na Ushauri (TUICO) ni miongoni mwa taasisi ambazo zimeanza safari ya nguvu kuelekea uwekezaji wa kidijitali na matumizi ya teknolojia ili kuboresha huduma kwa wanachama wake na kushirikiana vyema katika sekta zinazobadilika kwa kasi.
Wakati inapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, TUICO imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia hususani katika shughuli za kila siku. Mawasiliano, usajili wa wanachama na usimamizi wa taarifa za wanachama umekuwa ni wa kidijitali. Mabadiliko haya yanaonyesha jitihada za chama kwenda na wakati pia ikihakikisha majukumu ya kumtetea na kumlinda mfanyakazi yanafanyika kwa ufanisi.
Hapo awali, upatikanaji na utoaji wa taarifa ulitegemea nyaraka za karatasi. Hili lilichangia upotevu wa taarifa na matumizi ya muda mrefu kupata taarifa muhimu kwenye ngazi mbalimbali za Chama. Hivyo chama kikaanza matumizi ya mifumo ya kiteknolojia ili kutatua changamoto hii.
Mabadiliko makubwa yalianza mwaka 2017 kwa kuanzishwa kwa tovuti ya chama ambayo ilitambulisha uwepo wa TUICO mtandaoni na kutoa nafasi kwa wanachama na umma kupata taarifa kuhusu chama na shughuli zake bila kufika kwenye ofisi za mikoa au makao makuu ya chama. Uwepo huu mtandaoni uliimarishwa zaidi baada ya kuanzishwa kwa kurasa rasmi za mitandao ya kijamii.
Hili liliwezesha mawasiliano ya haraka zaidi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa. Pamoja na maboresho haya, TUICO ili kuongeza ufanisi wa utendaji katika kusajili na kutunza taarifa za wanachama kwa kuanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa (MIS), ambalo ni mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa taarifa za wanachama.
Kabla ya TUICO-MIS, kupata taarifa za mwanachama, kuthibitisha uanachama au kusahihisha taarifa kulichukua muda mrefu na ilikuwa ngumu. Lakini kwa sasa inawezekana kwa dakika chache. Hili limeongeza ufanisi mkubwa kwani kazi hiyohiyo hapo awali ilitumia masaa mengi.
Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe Ridhiwani Kikwete (katikati, walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wakati wa uzinduzi wa miongozo ya mifumo ya kielektroniki na majadiliano ya Serikali na vyama vya wafanyakazi na waajiri. TUICO ni moja ya vyama vilivyoshiriki uzinduzi huo uliofanyika Agosti mwaka huu.
Kwa kuwa ofisi zote zinatumia MIS, taarifa kutoka tawi lolote zinafikiwa mara moja katika ofisi ya mkoa na Makao Makuu kwa haraka na kwa wakati. Pia ripoti ambazo hapo awali zingechukua siku kuandaliwa sasa zinaweza kuandaliwa kwa dakika chache, hili limepelekea kuboresha upangaji, uratibu, na uwajibikaji. Hivyo matumizi ya teknolojia yaamebadilisha jinsi TUICO inavyosimamia taarifa za wanachama, na kufanya huduma kutolewa kwa haraka.
TUICO haijaishia kwenye kuanzisha na kutumia mifumo ya kidijitali pekee. Chama kimeendelea kuwajengea uwezo watendaji wake kote nchini jinsi ya kutumia mifumo na vifaa vya kidijitali kwa ufanisi, ili kuhakikisha kila mmoja anaweza kutoa huduma na kusimamia taarifa za wanachama kwa urahisi.
Wakati huo huo, TUICO pia imewekeza katika vifaa vya kisasa kama kompyuta, kompyuta mpakato (Laptop) na zana nyingine pamoja na kuunganisha mtandao (internet) kwenye ofisi zake zote ili kuendana na mabadiliko ya kitenolojia.
Hatua hizi zinahakikisha matumizi ya mifumo ya chama unaendelea kuimarika huku uwezo wa wafanyakazi, kufanya kazi kwa ufanisi unaongezeka na kuhakikisha wanachama wanapata huduma kwa wakati.
Kutokana na mapinduzi ya kidijitali Tanzania kuendelea kwa kasi ikiwa ni pamoja na ongezeko la watumiaji wa intaneti na matumizi ya huduma za 5G na huduma za Serikali mtandaoni, TUICO inaendelea kupanua uwekezaji wake wa teknolojia na kuboresha huduma kwa wanachama
TUICO imeanza safari muhimu ya uwekezaji wa kidijitali na matumizi ya teknolojia, kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya TEHAMA, kutumia majukwaa ya mtandao na mitandao ya kijamii, kusimamia taarifa kwa njia ya kidijitali, kuhamasisha elimu ya teknolojia kwa wanachama na kuchangia kwenye mabadiliko ya kijamii.
Kwa kuendelea kuboresha rasilimali hizi, chama kinajiweka katika mstari wa mbele wa vyama vya kisasa vinavyotumia teknolojia kukuza haki za wafanyakazi na ushiriki wa wanachama katika zama za digitali.