TIMU za KVZ na TRA United zilizopo Kundi C la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 ambalo pia linaijumuisha Yanga, zimetoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao 1-1.

Mechi hiyo iliyochezwa leo Desemba 29, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani hapa, ilionekana kuwa ya mashambulizi ya kushtukiza kila upande, huku kipindi cha kwanza kikimalizika bila ya kufungana.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Kocha wa TRA United, Etienne Ndayiragije, alifanya mabadiliko ya mapema dakika ya 28 kwa kumtoa Ramadhan Chobwedo na kuingia Abdulhamid Ramadhan.

Kuingia kwa Abdulhamid, kukaongeza nguvu eneo la pembeni ambapo dakika ya 54, kona aliyopiga ikaunganishwa vizuri kwa kichwa na Enock Mkanga, TRA United ikawa mbele kwa bao 1-0.

Bao hilo lilidumu kwa takribani dakika 12, baada ya Michael Joseph Godlove kuisawazishia KVZ.

Mshambuliaji wa TRA United, Adam Omary Adam, alionekana kuwa na hasira baada ya kufanyiwa mabadiliko akiwa amecheza kwa dakika 23 pekee. Alitokea benchi akiingia dakika ya 57 kuchukua nafasi ya James Msuva, kisha akatolewa dakika ya 80, nafasi yake ikachukuliwa na Shaban Idd Chilunda.

Matokeo hayo yanazifanya timu hizo kugawana pointi moja moja, ambapo Januari 4, 2026, KVZ itacheza dhidi ya Yanga, kisha Januari 6, 2026 zamu ya TRA United na Yanga. Kundi hili linatoa timu moja yenye pointi nyingi kwenda nusu fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *