
Admirali Ali Shamkhani, Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amelaani vikali vitisho vipya vilivyotolewa na Marekani vya kushambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu, akiapa kuwa jibu kali litatolewa endapo utafanywa uchokozi wowote ule.
Shamkhani ameyasema hayo katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii jana Jumatatu na kubainisha kwamba, kulingana na doktrini ya ulinzi ya Iran, majibu dhidi ya vitisho hupangwa kabla ya kutolewa vitisho hivyo.
Aidha, amesisitiza kuwa, uwezo wa makombora na wa ulinzi wa Iran hauwezi kuwekewa udhibiti au kutegemea ruhusa ya mtu yeyote.
Admirali Shamkhani ameonya kwamba uchokozi wowote dhidi ya Iran utakabiliwa na jibu kali na la haraka kuliko wanavyoweza kudhani wapangaji wake.
Jibu hilo limetolewa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kwamba ataunga mkono shambulio la utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Iran ikiwa Tehran itaendelea na mipango yake ya makombora ya balestiki na ya shughuli za nyuklia.
Trump alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mkutano wake na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu.
“Sasa nasikia kwamba Iran inajaribu kujenga tena, na ikiwa watafanya hivyo, itatupasa tuwaangushe,” alitamka Trump kuwaambia waandishi wa habari. “Tutawaangusha. Tutawaangusha vibaya. Lakini tunatumai hilo halitatokea.”
“ Kama tusingeishinda Iran, msingekuwa na amani Mashariki ya Kati,” amedai rais huyo wa Marekani katika moja ya matamshi yake.
Wakati huo huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeeleza katika taarifa liliyotoa jana hiyohiyo kwamba maadui wamedhamiria kupanda mbegu za uchochezi ndani ya jamii ya Iran kupitia vita vya utambuzi, operesheni za kisaikolojia, simulizi za uwongo, uenezaji hofu, na kushawishi taifa lisalimu amri mbele yao.
Katika taarifa yake hiyo, IRGC imevielezea vita vya kichokozi vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo mwezi Juni kama mfano bora wa tishio la mchanganyiko ambalo lilijumuisha wigo mpana wa kiusalama, kisaikolojia, na kiuchumi na kuvuka mpaka wa makabiliano ya kijeshi.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetahadharisha kuhusu majaribio yoyote ya kudhoofisha imani ya umma, likibainisha kuwa, hatua yoyote ya aina hiyo inaendana na malengo ya mataifa yenye kiburi duniani, yakiongozwa na Marekani na Israel.
Aidha, limetoa indhari kwa maadui ya kutojaribu kufanya mahesabu yoyote ya kimakosa, likisisitiza kwamba litalinda kwa nguvu kamili uhuru wa Iran, usalama, heshima na mamlaka yake dhidi ya kitendo chochote cha uchochezi, vita vya utambuzi, tishio la usalama, na uchokozi dhidi ya ardhi…/