Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetoa taarifa kali mno leo Jumanne ikiushutumu Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwamba unahatarisha usalama wa taifa na haki ya Saudia ya kuchukua maamuzi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, taarifa hiyo kali ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetolewa baada ya mamluki wa Imarati kufanya shambulio kali leo asubuhi dhidi ya mamluki wa Saudia katika majimbo ya Hadramaut na Al-Mahra ya kusini mashariki mwa Yemen.

Katika taarifa yake hiyo, Saudi Arabia imetangaza kwamba Imarati inatumia mashinikizo na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya wafuasi wa Saudia huko Yemen ili kulenga moja kwa moja usalama wa taifa wa Saudi Arabia.  Vitendo hivyo kwa mujibu wa Riyadh, ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa taifa wa Saudia pamoja na usalama na utulivu wa Yemen na eneo hili lote.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imezungumzia pia harakati za meli zilizobeba silaha na magari mazito ya kijeshi kutoka bandari ya Fujairah ya Imarati na kupelekwa kwenye bandari ya Mukalla nchini Yemen ikisisitiza kwamba, hatua hiyo imechukuliwa na Muungano wa Falme za Kiarabu bila ya kushauriana na wafuasi wa Saudi Arabia nchini Yemen. Riyadh inaihesabu hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya huko nyuma ya pande hizo mbili kuhusu Yemen.

Katika sehemu muhimu ya taarifa hiyo, Saudi Arabia imeeleza kuwa, vitendo vya Imarati ni vya “hatari sana” na kufafanua kwamba tabia hizo za Abu Dhabi zinavuruga juhudi za kuleta usalama na utulivu za Saudia.

Riyadh imeonya vikali kwa kusema: “Uchokozi wowote au tishio lolote dhidi ya usalama wa taifa wa Saudi Arabia ni mstari mwekundu, na Utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia hautosita kuchukua hatua zozote muhimu za kukabiliana na uchokozi kama huo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *