Mwaka 2025 haukuwa wa kawaida kwa Tanzania. Haukuwa mwaka wa matukio ya kawaida pekee, bali ulikuwa mwaka wa mpito, tafakari na majaribio makubwa ya kisera.

Ni mwaka ambao matumaini ya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu yalikutana uso kwa uso na uhalisia wa shule, vyuo, walimu, wanafunzi na kaya nyingi za Kitanzania.

Halikuwa jambo la siri, kuanzia Januari hadi Desemba, elimu ilijikuta ikitawala vichwa vya habari, mijadala ya kisiasa, mikutano ya kitaalamu, mijadala ya redio na televisheni, pamoja na mazungumzo ya kawaida ya wazazi mezani.

Kwa namna nyingi, mwaka huu uliiweka elimu katika mizani ya taifa,  kati ya ndoto ya elimu inayobadilisha maisha na changamoto sugu za utekelezaji.

Mwaka ulianza kwa msisimko mkubwa wa mjadala wa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya toleo jipya. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliweka wazi dhamira ya kuibadili elimu ya Tanzania kutoka mfumo unaojikita katika kukariri kwenda kwenye ujuzi, ubunifu, fikra tunduizi na maandalizi ya moja kwa moja ya soko la ajira.

Katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Elimu, hoja za matumizi ya Tehama, akili bandia na pengo la elimu kati ya mijini na vijijini ziliibuka kwa nguvu mpya. Wataalamu walikiri kuwa dunia ya kazi inabadilika kwa kasi kuliko mifumo ya elimu.

Hata hivyo, sauti kutoka mashinani zilirejesha uhalisia. Mwalimu wa shule ya sekondari kutoka Rufiji alinukuliwa akisema, “Sera ni nzuri, lakini shule yangu haina hata umeme wa uhakika, sembuse teknolojia.”

Februari: Mtaala mpya wazua maswali

Februari ulitawaliwa na mjadala mzito kuhusu uwezo wa walimu kuhimili mtalaa mpya. Vyama vya walimu vilionya kuwa kasi ya mageuzi haijaendana na maandalizi ya walimu wala mazingira halisi ya shule nyingi za umma.

Hoja za upungufu wa walimu wa sayansi na hesabu, msongamano wa wanafunzi darasani, pamoja na uhaba wa vitendea kazi zilijirudia mara kwa mara. Mwalimu wa sayansi kutoka Tabora, Mery Emmanuel alisema: “Tunafundisha kwa ari na uzalendo, lakini hatujaandaliwa vya kutosha kwa mtalaa huu unaohitaji vitendo zaidi kuliko nadharia.”

Machi: Matokeo ya mitihani na ubora

Matokeo ya mitihani ya taifa yaliporejeshwa mezani, mjadala wa ubora wa elimu ulirudi kwa nguvu. Tofauti kati ya shule za binafsi na za umma ilionekana wazi, huku baadhi ya mikoa ikitajwa kuwa na viwango vya ufaulu visivyoridhisha.

Wataalamu wa elimu walieleza kuwa tatizo si wanafunzi pekee, bali mfumo mzima unaowazunguka. Wazazi walirejesha hoja ya nidhamu, malezi na mchango wa familia katika safari ya elimu.

Mzazi mmoja jijini Mwanza John Mponji alisema kwa masikitiko: “Shule peke yake haiwezi kulea, familia imetelekeza wajibu wake.”.

Mei: Bajeti ya elimu chini ya darubini

Kadri mjadala wa bajeti ya Serikali ulipokaribia, sekta ya elimu iliwekwa chini ya darubini kali. Wadau walitaka kuona ajira mpya za walimu, ujenzi wa madarasa na mabweni, uendelevu wa sera ya elimu bila ada, pamoja na uboreshaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na Mwalimu mstaafu kutoka mkoani Mtwara Dkt Azikiwe Boraufe alieleza kuwa, bajeti ya elimu si matumizi ya kawaida, ni uwekezaji wa muda mrefu wa kizazi kijacho.

Juni ulikuwa kilele cha mjadala wa elimu. Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliposomwa bungeni, ilisisitiza ujenzi wa miundombinu, mageuzi ya mtalaa, matumizi ya Tehama na kuimarisha elimu ya amali na ufundi.

Hata hivyo, mjadala haukuishia bungeni. Katika jamii, swali lilibaki lilelile: je, rasilimali zilizotengwa zinatosha kubeba mabadiliko makubwa yanayotarajiwa?

Agosti: Elimu ya ufundi yajitokeza kama suluhisho

Agosti ulirejesha kwa nguvu mjadala wa elimu ya ufundi stadi. Vyuo vya VETA, wataalamu wa soko la ajira na sekta binafsi walisisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo.

Mwajiri katika sekta ya ujenzi jijini Dar es Salaam Benard John alisema: “Tunahitaji vijana wenye ujuzi wa kazi halisi, si vyeti pekee vinavyopamba mafaili.”

Septemba: Shule zafunguliwa, changamoto zasalia

Shule zilipofunguliwa tena, changamoto za muda mrefu zilirejea kana kwamba hazijawahi kuondoka. Uhaba wa walimu, msongamano wa wanafunzi, upungufu wa vitabu na madarasa machache viliripotiwa tena.

Huu ulikuwa mwezi uliorejesha mjadala mpana kuhusu kama elimu bila ada inaendana kikamilifu na lengo la kuboresha ubora wa elimu.

Oktoba: Elimu na siasa zakutana

Katika mazingira ya uchaguzi mkuu, elimu ikawa ajenda muhimu ya kisiasa. Vyama vya siasa vilitoa ahadi kuhusu ajira za walimu, mikopo ya elimu ya juu, mtalaa na lugha ya kufundishia.

Kwa wapiga kura wengi, elimu ikawa ishara ya matumaini, lakini pia chanzo cha wasiwasi kuhusu utekelezaji wa ahadi hizo baada ya uchaguzi.

Novemba: Tathmini ya mwaka

Novemba ulikuwa mwezi wa kuangalia nyuma. Makala za tathmini zilijaa katika vyombo vya habari, zikibeba sauti za walimu, wanafunzi, wazazi na wataalamu wa elimu.

Walimu walizungumza kwa uchungu kuhusu mazingira ya kazi, wanafunzi walieleza changamoto za ujifunzaji, wazazi walilalamikia gharama zisizo rasmi, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa uwiano kati ya sera, bajeti na utekelezaji. Swali kuu likabaki je, huu ulikuwa mwaka wa mabadiliko ya kweli au maandalizi ya mabadiliko?

Desemba: Tafakari na dira ya mwaka ujao

Desemba ulihitimisha mwaka kwa tafakari nzito ya kitaifa. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alipokutana na wanahabari, aliweka wazi mwelekeo wa Serikali kwa mwaka unaofuata.

Alizungumzia mpango wa kuwapeleka wanafunzi 50 nje ya nchi kusomea sayansi, kuimarisha Samia Scholarship Fund, pamoja na kurasimisha mafundi mchundo ili ujuzi wao utambulike rasmi katika mfumo wa elimu na ajira.

Kwa wengi, kauli hiyo ilirejesha matumaini mapya. Mtaalamu mmoja wa elimu ya ufundi alisema: “Kurasimisha mafundi mchundo ni kukiri kuwa elimu ipo pia nje ya madarasa.”

Mwisho wa mwaka 2025, Tanzania ilibaki na funzo moja kubwa, kwamba elimu ni safari ndefu inayohitaji zaidi ya sera, bajeti na ahadi. Inahitaji uhalisia, ushirikishwaji wa wadau wote na dhamira ya pamoja ya kitaifa ya kuifanya elimu kuwa injini ya maendeleo, si mzigo wa majadiliano yasiyoisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *