
Kwa nini siku zinakwenda kasi? Majuzi tu tumesherehekea Mwaka mpya wa 2025, na leo tumeshauzoea mwaka mpya mwingine wa 2026. Kajukuu kangu kalikokuwa kakiniomba Shilingi Ishirini kakanunue kipande cha kaukau, ati kameshachukua Shahada ya Uzamivu katika Udaktari. Mara hii kameshakua kajitu kazima!
Hivi karibuni tu niliweka lengo la kuwanunulia watoto viwanja. Si kwa ajili ya makazi, bali kwa ajili ya kujifunza michezo ya asili. Watoto wa siku hizi wanakosa mengi kwa sababu ya kucheza mpira kwenye kompyuta. Labda wanajiandaa kucheza Kombe la Dunia la Kompyuta!
Katika ramani yangu niliweka eneo la kucheza “kombolela”, “kula umbakishie baba”, “tobo ngumi” na michezo mingi mingineyo. Nilikamilisha mambo matatu katika awamu ya kwanza ya utekelezaji: Kuliteua (sio kulinunua) eneo, kutengeneza jina la mradi na sikupata taabu kumpata mkufunzi. Niliteua shamba kule Buza, kisha nikaupa jina mradi kuwa “Ujenzi wa Kijiji cha Michezo.
Sikuumiza kuchwa kutafuta mwalimu wa michezo ya watoto. Mke wangu Bi. Mlevi anazo sifa zote za kuwa msimamizi mkuu wa kijiji changu. Anao uzoefu wa miaka miaka mingi katika michezo hiyo, hata sasa nisipomnunulia mafuta ya kupaka hukumbuka kucheza.
Tangu alipoacha biashara ya Kangara (a.k.a. “Pombe Gani”) amekuwa akiendesha vikundi vya kufaana vya akinamama yeye akiwa Kijumbe. Lakini kwa vile amekwisha kukoswakoswa kung’olewa meno na wenzake mara nyingi, nikamdokeza kuhusu mradi huu. Aliupokea kwa mikono miwili, japo hataki kuniambia mkono mmoja uliofungwa hogo umefanywa nini.
Leo ninakumbuka kuwa sijatimiza awamu ya ujenzi wa kijiji hicho. Changamoto zilikuwa nyingi kiasi kwamba ikawa vigumu kufikia malengo kwa muda uliopangwa. Kumbuka kuwa bajeti ya mradi mzima ilianza pale bia ilipouzwa Shilingi Mia Mbili na Hamsini. Mwendokasi wa bei ya kinywaji hicho ulitengeneza mwendokasi wa ukaukaji wa mifuko yangu. Kazini kwangu waligoma kunipa posho ya kinywaji.
Leo ninamwita mjukuu wangu Kisoda ili niitetee sera yangu, na kumpa matumaini kuwa akinichagua tena kwa awamu ingine… Ah! sorry, akiniamini kwa mwaka huu tu, hakika nitatimiza ndoto zake za kuwa kijana atakayejitambua hapo baadaye.
Kisoda aliposimama mbele yangu ninapigwa na butwaa. Kumbe huyu ndiye aliyetunukiwa shahada yake ya Uzamivu! Ama kweli siku zinakimbia. Yaani kama vile Nzaeli Kyomo alivyomaliza mbio za mita mia moja kwa sekunde chache, au kama bongofleva iliyoimbwa juma la jana inavyoitwa zilipendwa juma hili. Yaani huyu aliyekuwa kichanga juzi tu, leo anaitwa daktari bingwa!
Siku zinakimbia hadi historia inapitwa. Zamani ungeona makombo ya mwaka jana, lakini sasa tazama kama utaona miti ya Krismasi iliyotupwa. Zamani miti ya Krismasi ilizunguka uwanja. Hadi mbwa aliandaliwa wa kwake! Lakini ni siku zinakimbia au sisi ndio tunakimbia? Yawezekana kabisa upepo unaofukuta mifukoni ndio unaotutia uchizi wa kwenda kasi namna hii. Wapi methali ya “Polepole Ndio Mwendo”?
Wajamaika wa miaka ya Sabini na Themanini walikuwa na msemo wao: “A house is not a home without a Television” (nyumba haiwezi kuwa nyumbani kukikosekana runinga). Ilikuwa ni baada ya kujiona kuwa wapo huru na wanaweza kujiachia watakavyo. Waliweza kuvuka kwa urahisi kwenda kufanya vibarua Ulaya na Marekani. Kwa nini washindwe kununua TV?
Bibi Mlevi naye kaja na yake. Kataka king’amuzi, nikamnunulia. Kataka deki, nikamletea. Lakini tukaingia kwenye mzozo mpya. Ninapojiandaa kuangalia taarifa ya habari, rafiki zake walikuja na mix grill; mmoja alikuwa na DVD (wenyewe wanaita mikanda) za kitchen party za mjukuu wa shoga zake, na wengine wawili au watatu waliingia na DVD za tamthilia walizonunua Shilingi Mia Tano (zaga) pale Buguruni.
Niliona aibu kumsusia mke wangu, hivyo nilijilazimisha kubaki na jino langu la pembe. Ubaya ni kwamba Bibi Mlevi alinihadithia kila kilichoendelea kwenye zile video. Tena bila huruma akawa akiniandaa; “Basi hapo ataingia Mama Sijali kumwaga lazi…” Wiki ile sikuwa kama mgonjwa, bali nilikuwa ni zaidi ya mgonjwa. Shetani akanishauri kuihujumu deki ya DVD.
Sikuiharibu, ila nilibadilisha nyaya tu: wa picha nikaweka kwenye sauti na wa sauti kwenye picha. Kwa siku tatu niliishi kwa amani. Lakini kumbe nilifanya jambo baya hadi nikaujutia ubunifu wangu. Ilikuwa siku ya nne nilipowahi kurudi ili nijiandae kwa safari ingine. Nikalikuta jopo la Bibi Mlevi likiwa limeizunguka ile deki: “Hakuna bwana,” mmoja aliyeshika nyundo alipaza sauti, “Mume wangu alikigongagonga tu, ikawaka.”
Astakafiru! Kufumba na kufumbua deki ikagongwagongwa nikashindwa hata kuitazama. Sikusema lolote zaidi ya kugeuka na kuondoka. Lakini Bibi Mlevi aliniona na kuniwahi. “Ukienda huko urudi na deki. Lakini safari hii niletee ya Kituruki!” Nilimsikia kwa sababu ilibidi kumsikia, lakini sikumwelewa.
Niliporudi bila deki nikawa na mzozo mwingine tena. Alivizia muda ambao usingizi ndio ulikuwa unanianza, yeye akawasha busta kwa sauti ya juu. Na kibaya zaidi mwenyewe aliimba kwa sauti mbaya na kubwa zaidi akiusindikiza wimbo: “Mai switi switi, Mai VIDEOOOOO…” Ah! Roho yangu jamani.