Rabat, Morocco. Wenyeji Morocco wameendeleza ubabe wao katika Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya jana kuifunga Zambia mabao 3-0 na kumaliza kileleni mwa Kundi A, huku Mali na Afrika Kusini nazo zikifuzu hatua ya mtoano.
Morocco imemaliza kwa kwa kishindo mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Zambia, matokeo yaliyowawezesha kumaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi saba.
Shujaa wa mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, alikuwa Ayoub El Kaabi aliyefunga mabao mawili, likiwemo bao la kuvutia alilopachika kipindi cha pili.
Bao la kwanza liliingia mapema dakika ya tisa baada ya mpira wa kona uliopigwa na Azzedine Ounahi, El Kaabi alipaa juu na kupiga kichwa kilichozama wavuni.
Morocco iliongeza bao la pili dakika ya 27 kupitia Brahim Diaz aliyemalizia pasi ya Abde Ezzalzouli, kabla El Kaabi kufunga bao lake la pili dakika ya 53, VAR ikithibitisha bao hilo baada ya awali kuonekana kama ameotea.
Akizungumza baada ya mchezo, El Kaabi aliyechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi amesema:
“Lengo letu lilikuwa kumaliza kileleni na tumelitimiza. Sasa tunajiandaa kwa hatua ya mtoano ambako hakuna nafasi ya makosa.”
Kocha wa Morocco, Walid Regragui, amesema mpango wao wa mchezo ulifanya kazi ipasavyo na kusisitiza kuwa kila mchezo kwao ni kama fainali.
Kwa upande wa Zambia, kocha Moses Sichone amekiri timu yake ilicheza kwa hofu na kushindwa kuhimili presha.
Mali yasonga mbele
Mali imefanikiwa kusonga mbele baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Comoros katika mchezo uliokuwa na presha kubwa. Sare hiyo iliitosha Mali kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi hilo kwa pointi tatu baada ya sare tatu mfululizo.
Comoros walionyesha ushindani mkubwa hasa kupitia mashambulizi ya kushtukiza, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata. Mali walimaliza mchezo wakiwa pungufu baada ya Amadou Haidara kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 88.
Matokeo hayo yameifanya Comoros kumaliza nafasi ya tatu kwa pointi mbili, jambo lililowafanya kuaga mashindano.
Angola yakwaa kisiki
Angola imeshindwa kupata matokeo baada ya kulazimishwa sare na Misri katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade Adrar. Ingawa Angola walionekana kuwa bora hasa kipindi cha pili, walishindwa kupata bao kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Misri.
Fredy ambaye ni kiungo wa Angola alitangazwa Mchezaji Bora wa Mechi, akisema kuwa huo ulikuwa mchezo wake wa mwisho kuitumikia timu ya taifa baada ya miaka 12.
Kocha wa Misri, Hossam Hassan, amesema sare hiyo inawatosha na tayari wamejipanga kwa hatua ya 16 bora.
Bafana Bafana yafuzu
Afrika Kusini ilifuzu hatua ya mtoano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Zimbabwe katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa hadi dakika za mwisho.
Bafana Bafana walitangulia kufunga mapema kupitia Tshepang Moremi, kabla Zimbabwe kusawazisha kwa bao la kuvutia la Tawanda Maswanhise. Lyle Foster aliirejesha Afrika Kusini mbele, Oswin Appollis akafunga bao la penalti dakika ya 82.
Zimbabwe walipunguza tofauti kupitia bao la kujifunga, lakini juhudi zao za kusawazisha hazikuzaa matunda.
Kocha wa Afrika Kusini, Hugo Broos, amesema timu yake bado ina changamoto za kiulinzi licha ya ushindi huo, huku kocha wa Zimbabwe Mario Marinica akisema makosa madogo yaliwagharimu.
Kwa ushindi huo, Afrika Kusini imemaliza nafasi ya pili Kundi B kwa pointi sita, Zimbabwe ikimaliza mkiani kwa pointi moja.
Timu zilizofuzu hatua ya mtoano
Afrika Kusini