s

Chanzo cha picha, aviationa2z/General Atomics Aeronatuical Systems

Muda wa kusoma: Dakika 4

Marekani imechukua hatua mpya na ya kimkakati kwa kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Caribbean, safari hii si kwa kupeleka askari au manowari, bali kwa kutumia teknolojia ya juu ya ndege zisizo na rubani. Hatua hii imekuja wakati changamoto za usalama wa mipaka na biashara haramu ya dawa za kulevya zikizidi kuhitaji mbinu za kisasa na zenye ufanisi zaidi.

Jeshi la Anga la Marekani (U.S. Air Force) limethibitisha kuongezwa kwa idadi ya ndege zisizo na rubani aina ya MQ-9A Reaper, zinazofanya operesheni zake kutoka Uwanja wa ndege wa Rafael Hernández, Aguadilla, nchini Puerto Rico. Kwa mujibu wa taarifa rasmi na picha zilizochapishwa hivi karibuni, sasa kuna ndege saba za aina hii zinazofanya kazi katika eneo hilo, ishara ya wazi ya kuimarika kwa ufuatiliaji wa anga.

Hatua hii inaonesha mabadiliko ya wazi katika mkakati wa usalama wa Marekani kutoka utegemezi wa ndege zenye marubani kwenda kwenye mifumo ya kisasa ya ujasusi wa anga inayoweza kufanya kazi kwa muda mrefu, kwa gharama ndogo na bila kuhatarisha maisha ya binadamu.

Kwa wengi, jina MQ-9A Reaper linaibua taswira ya mashambulizi ya kijeshi katika maeneo ya migogoro. Hata hivyo, katika operesheni za Caribbean, ndege hii imetumwa hasa kwa ajili ya upelelezi, ufuatiliaji na ukusanyaji wa taarifa muhimu za kiusalama. Lakini ni ndege ya aina gani hasa? Na kwanini inatajwa kuwa hatari zaidi duniani?

MQ-9A Reaper ni ndege ya aina gani?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

MQ-9A Reaper ni ndege ya kisasa isiyo na rubani (unmanned aerial vehicle – UAV) iliyotengenezwa na kampuni ya Marekani ya General Atomics Aeronautical Systems. Ndege hii ni ya matumizi mengi, ikiwa imeundwa kufanya kazi za ujasusi, ufuatiliaji, na pale inapohitajika, mashambulizi ya kijeshi.

Kwa muundo wake, Reaper ina mabawa yenye upana wa takribani mita 20, na uzito wa juu wa kuruka unaofikia karibu kilo 4,760. Ina injini yenye nguvu inayoiwezesha kuruka katika urefu wa hadi futi 50,000, juu zaidi kuliko ndege nyingi za kiraia na baadhi ya ndege za kijeshi.

Moja ya sifa kuu za MQ-9A Reaper ni uwezo wake wa kukaa angani kwa muda mrefu sana. Kutegemea mzigo wa vifaa ilivyobeba, droni hii inaweza kukaa angani kwa zaidi ya saa 40 mfululizo, ikifanya doria na kukusanya taarifa bila kusitishwa. Hii ni faida kubwa ukilinganisha na ndege zenye marubani, ambazo zina mipaka ya muda kutokana na uchovu wa binadamu.

Teknolojia na uwezo wake wa kijasusi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Kinachoifanya MQ-9A Reaper kuwa chombo muhimu sana si ukubwa wake pekee, bali ni teknolojia ya hali ya juu iliyobebwa ndani yake. Ndege hii ina mifumo ya kisasa ya sensa zinazoiwezesha kufanya kazi mchana na usiku, katika hali zote za hewa.

Reaper imefungwa kamera za video (full-motion video camrea) zinazoweza kufuatilia maeneo yanayofuatiliwa kwa wakati halisi, sensa za infra-red kwa ajili ya kuona vitu hata gizani, pamoja na rada ya synthetic aperture inayoweza kugundua vyombo vidogo baharini au ardhini, hata vinapojaribu kujificha.

Katika eneo la Caribbean, teknolojia hii hutumika kufuatilia njia za baharini zinazotumiwa kusafirisha dawa za kulevya. Reaper inaweza kutambua boti ndogo za kasi (go-fast boats), vyombo vingine (semi-submersible) na meli ndogo zinazojaribu kupita bila kugunduliwa.

Taarifa zote hukusanywa na kupelekwa moja kwa moja katika mitandao ya kijasusi ya Marekani kwa wakati halisi na kuwasilishwa kwa vikosi vingine vya kijeshi na vyombo vya sheria. Hii hurahisisha maamuzi ya haraka na uratibu wa operesheni za kukamata au kuzuia shughuli haramu.

Kwanini MQ-9A Reaper inatajwa kuwa hatari zaidi?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Sababu kuu inayofanya MQ-9A Reaper kutajwa kama “drone hatari zaidi duniani” si kwa sababu ya upelelezi wake pekee, bali pia kwa uwezo wake wa kubeba silaha. Ingawa operesheni za Caribbean kwa sasa ni za ujasusi tu, Reaper imeundwa kubeba silaha za kisasa zenye usahihi mkubwa.

Kitaalamu, MQ-9A Reaper inaweza kubeba makombora yanayoongozwa kwa teknolojia ya hali ya juu, yanayoweza kulenga shabaha kwa usahihi mkubwa bila kuharibu maeneo ya pembeni. Uwezo huu huifanya kuwa chombo cha kutisha katika mazingira ya kivita.

Zaidi ya silaha, hatari ya Reaper iko katika mchanganyiko wa muda mrefu wa doria, ufuatiliaji wa karibu na ukusanyaji wa data kwa wakati halisi. Adui au mtandao wa uhalifu anaweza kufuatiliwa kwa masaa au hata siku bila kujua, hadi pale hatua itakapochukuliwa.

Kwa kutumia drone badala ya askari au ndege zenye marubani, Marekani pia inapunguza hatari ya vifo vya binadamu, huku ikiendelea kudhibiti maeneo makubwa kwa ufanisi mkubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *