
Kipindi hiki kinachunguza kwa makini nafasi ya vyombo vya habari vya Hollywood na mitandao ya habari yenye uhusiano na taasisi zenye nguvu na madaraka huko Marekani, hasa kampuni ya utengenezaji filamu ya Millennium Media, katika kujenga upya, kutakatisha sura ya Marekani na kuhalalisha sera zake za kuingilia kati masuala ya nchi nyingine duniani. ********
Kwa kawaida, tunapozungumzia nguvu ya nchi, akili zetu huelekea kwenye jeshi, uchumi na teknolojia. Lakini ukweli ni kwamba hakuna nguvu katika ulimwengu wa leo inayoweza kuishi bila kudhibiti picha, taswira na simulizi za vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tasnia ya filamu. Katika ulimwengu wa kisasa, picha ni muhimu zaidi kuliko uhalisia na ukweli wa mambo. Anayeandika habari na simulizi huunda uhalisia. Na katika suala hili, Marekani ndiyo kinara asiye na kifani katika kutengeneza na kubuni simulizi tofauti na uhakika na uhalisia wa mambo.
Marekani haitawali pande nyingine kwa kutumia silaha na meli za kivita tu; bali pia huzishinda na kuzidhibiti akili kwa kutumia wenzo wa sinema, mitandao ya habari, studio za filamu na kampeni ya vyombo vya habari.
Kuanzia Hollywood hadi mitandao ya habari, utengenezaji wa vipindi vya burudani hadi utayarishaji wa filamu za ducumentary zenye mwelekeo maalumu, yote hayo hufanya kazi kwa pamoja ambayo ni kukarabati na kutakatisha sura ya Marekani kama mhubiri wa uhuru, mwokozi wa ulimwengu na nguvu pekee halali ya mamlaka. Ndiyo! Marekani inadumisha, kulazimisha na kuimarisha taswira yake kwa kuzalisha maelfu ya filamu, vipindi vya televisheni, tamthilia, documentary zenye mwelekeo maalumu na kuzindua mitandao ya habari duniani. Katika mchakato huo, Marekanii daima hujipa nafasi ya “mwokozi” ambaye bila yeye ulimwengu unaonekana kuporomoka na kuelekea kuzimu. Lakini je, ukweli ukoje ikilinganishwa na picha hii inayotolewa na kusimuliwa na vyombo vya habari vya Marekani?
Mmoja wa wahusika wakuu katika “ufalme” huu wa kubuni na kutengeneza taswira na simulizi ni kampuni ya utengenezaji filamu ya Millennium Media. Kwa miaka mingi, kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza filamu ambapo shujaa Mmarekani, – mara nyingi akiwa amejeruhiwa na peke yake, lakini mwenye roho isiyokubali kushindwa, -huingia uwanjani na kupigana na kile kinachotajwa kuwa “nguvu za shari na uovu.” Kidhahiri, jambo hili huonekana kama burudani tu, lakini kwa hakika, huwa ni simulizi ya kisiasa kuhusu nafasi ya Marekani duniani.
Millennium Media na makampuni mengine kama hii, si kampuni ya utengenezaji filamu tu, bali pia ni sehemu ya nyenzo za diplomasia laini (soft diplomacy) za Marekani. Makampuni haya, ambayo yana historia ya kutengeneza filamu nyingi za aksheni na mapigano zenye bajeti kubwa, kwa miaka mingi yamemtambulisha shujaa Mmarekani duniani kwa sura ya askari, polisi au mtu anayepigana dhidi ya “uovu.” Lakini swali kuu linaloulizwa ni kwamba: Nani anaarifisha na kufafanua maana ya “uovu”? Na kwa nini Marekani siku zote huwa “mwokozi” katika filamu hizo? *********
Kwanza hebu tuitazame kampuni kubwa ya Marekani ya Millennium Media.
Millennium Media ni mojawapo ya studio mashuhuri zaidi za filamu nchini Marekani yenye makao yake makuu mjini Los Angeles na imekuwa maarufu kwa kutengeneza filamu za aksheni na mapigano za gharama kubwa katika upeo wa kimataifa. Katika miongo miwili iliyopita, kampuni hiyo ilikuwa na nafasi kubwa katika utengenezaji wa filamu kama vile The Expendables, Rambo, Angel Has Fallen na London Has Fallen; kazi ambazo, ukiangalia kijuujuu, huonekana kama bidhaa za burudani tu, lakini kwa hakika zina kitu kimoja kinachofanana. Katika filamu zote hizo, Marekani inadhihirishwa kama “mwokozi” na “mlinzi” au mtetezi wa nidhamu na mfumo wa kimataifa.
Kwa mtazamo wa kwanza, suala hili linaweza kuonekana kama chaguo la hadithi tu, lakini tunapochunguza kwa undani mwelekeo unaojirudia wa simulizi hizi, kunajitokeza muundo na kigezo kimoja cha wazi. Katika filamu hizi, dunia huoneshwa kuwa inakaribia kuporomoka, kutumbukia kwenye machafuko, au kukabiliwa na tishio. Nchi, serikali na hata viongozi wa dunia wanaonyeshwa kama wafisadi wasio na ufanisi, au walionaswa katika dimbwii la machafuko. Wakati huo, ni taifa moja tu lenye uwezo wa kuingilia kati na kurekebisha hali hiyo: Marekani. Huu ndio muundo wa kawaida wa simulizi laini ya Marekani.
Ni muhimu kutambua kwamba, Millennium Media haiimarishi tu simulizi inayoitambulisha Marekani kama “mwokozi”, bali pia hufafanua upya na kuarifisha “adui” katika kazi zake nyingi. Wakati mmoja, adui huyo huwa Asia Magharibi, ambayo Marekani inasisitiza kuiita Mashariki ya Kati. Na wakati mwingine, Russia, Amerika Kusini, au makundi vya Muqawama. Kwa maneno mengine ni kwamba, kampuni hii haisemi tu kwamba Marekani ni shujaa, bali pia inafafanua, ni nani anayepaswa kutambuliwa kuwa adui katika akili za hadhira ya kimataifa.
Uchunguzi wa miradi ya kampuni hiyo kwa undani unaonyesha kwamba filamu zake nyingi hutengenezwa kwa ushauri wa moja kwa moja kutoka wanajeshi wa Marekani na vyombo vya usalama. Hiki ndicho kigezo ambao kimekuwepo kwa miaka mingi katika ushirikiano kati ya Hollywood na Pentagon: Vyombo vya habari vinaunda, nguvu ya kijeshi inaunga mkono ili simulizi hiyo ijikite katika bongo na akili za jamii ya kimataifa.
Tunapaswa kusema kuwa, Millennium Media sio studio ya filamu tu, bali ni chombo cha simulizi yenye malengo ya kisiasa. Ni chombo kinachosaidia kuhakikisha kwamba ulimwengu unaiona Marekani si kama mhusika mkuu katika kusababisha migogoro, bali kama shujaa katika kutatua machafuko na migogoro hiyo. Kwa mfano tu, iwapo uingiliaji kati wa kijeshi wa Marekani katika nchi fulani utashindwa au kusababisha mporomoko wa kiuchumi na kijamii, simulizi ya vyombo vya habari husema: “Nchi hii ilikuwa na matatizo tangu mwanzo. Marekani imejaribu tu kusaidia.” Hapa ndipo sinema inapounganishwa na siasa.
Ili kuelewa ipasavyo maudhui hii, lazima turudi kwenye dhana ya nguvu laini (Soft Power). Neno hilo liliingizwa kwa mara ya kwanza katika fasihi ya kisiasa na mnadharia wa Marekani, Joseph Nye. Nguvu laini ina maana ya: Uwezo wa kuunda na kuelekeza maoni na imani za watu wengine bila kulazimishwa au kutumia mabavu. Sinema na vyombo vya habari ndio kituo kikuu cha nguvu laini, (Soft Power). Hebu tuangalie mifano halisi ya suala hili:
Wakati wa Vita vya Iraq vya 2003, Marekani iliimbia dunia kwamba, “Tunaenda kuwakomboa watu wa Iraq na kutokomeza silaha za maangamizi makubwa.” Baadaye, Wamarekani wenyewe walikiri kwamba hakukuwa na silaha za aina hiyo nchini Iraq. Hata hivyo vyombo vya habari vilikuwa tayari vimefanya kazi yao, na picha ya “mapambano ya kupigania uhuru” ilikuwa imechorwa katika akili za walimwengu.
Mfano mwingine ni mashambulizi na uvamizi wa Marekani huko Afghanistan, Libya, Syria, Amerika Kusini, Venezuela, Cuba na Nicaragua. Katika kila moja ya nchi hizi, vyombo vya habari vya Marekani na washirika wake vilitoa simulizi moja inayofanana: kwamba Marekani ni “mkombozi”. Watu wanaihitaji. Upande mwingine ni shari na uovu. Hiki ndicho kigezo kinachofuatwa cha propaganda.
Ili kujitakatisha, Marekani imetengeneza maelfu ya filamu kuhusu mashambulizi yake dhidi ya nchi zingine, kuonyesha jinsi ilivyokuwa “mwokozi” wa nchi hizo, kupindisha ukweli na kujifanya shujaa.
Kampuni ya Millennium Media ina nafasi kubwa sana katika kutengeneza “Shujaa Mmarekani” (American Hero). Filamu za kampuni hii kwa kawaida hujumuisha vipengele vifuatavyo:
1. Shujaa Mmarekani anayekuwa peke yake lakini mwenye nguvu
2. Adui asiye na sura au shetani (Mwarabu, mtu wa Mashariki mwa dunia, Mrusi au Mwislamu).
3. Kuhalalisha uvamizi na utumiaji mabavu wa Marekani kama “dharura kwa ajili kuokoa ulimwengu” na kadhalika. Taswira hii hufanya vita vya Marekani vionekane kama suala la kibinadamu.
Lakini suala hili haliishi katika tasnia ya sinema na filamu tu. Habari, mitandao ya kijamii, televisheni za kimataifa kama CNN, BBC, na FOX NEWS, zote huzalisha masimulizi wenye mwelekeo maalumu kwa wakati unaofaa. Vyombo hivi haviripoti tu, bali vinabuni na kutoa mwelekeo maalumu. Huamua ni nini habari, kipi kionyeshwe na kuonekana, na kipi kinapaswa kupuuzwa, kuchujwa au kufichwa kabisa. Kwa mfano, hadi hivi karibuni huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, ukweli halisi ulionekana wazi, lakini simulizi ya vyombo vya habari vya Marekani ilikuwa jambo lingine. Ulimwengu ulishuhudia kilichokuwa kikiendelea, lakini vyombo vya habari vilibadilisha “fremu” na kubuni simulizi tofauti. Neno “haki ya Israel ya kujilinda” lilibuniwa na kuchukua nafasi ya mauaji ya halaiki ya watu wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina. Hii ndiyo nguvu ya simulizi.
Simulizi inayowasilishwa na Marekani imeigawa dunia katika sehemu mbili: Marekani na wengine. Hao ‘wengine’ wasiokuwa Marekani kwa kawaida huarifishwa kuwa “wasio imara,” “hatari, “waliobakia nyuma,” au “dhidi ya uhuru.” Kwa msingi huo ni “halali” kwa Marekani, “mwokozi”, kuvamia nchi hizo, kuingilia kati, kuzishambulia kwa mabomu, kuzikalia kwa mabavu na kuvidhihirisha vitendo hivi si kama uchokozi, bali kama uokozi.
Kwa hivyo swali halisi si kile ambacho Marekani inafanya, bali ni: Inafanyaje ili kile inachokifanya kionekane sawa, cha kibinadamu na cha lazima?
Hapa ndipo utakatishaji wa vyombo vya habari vya Marekani unapofanyakazi. Hapa ndipo Millennium Media na studio zingine washirika zinapoingia kwenye medani na uwanja. Ili kuweka wazi suala hili, ni vyema kuelezea mihimili minne mikuu ya simulizi hizi:
Kuna mtindo na kigezo kimoja cha kufuatwa katika filamu zote za Marekani na hata katika habari na uchambuzi wa vyombo vikuu vya habari. Katika mfumo huo, ukweli huwa ni kinyume na tofauti kabisa na simulizi:
1. Ukweli ni kwamba: Marekani huanzisha vita, lakini simulizi ya vyombo vya habari huwaambia walimwengu kwamba Marekani huingia vitani kwa ajili ya kutetea uhuru na ubinadamu.
2. Ukweli na uhakika unaonyesha kuwa, watu wasio na hatia ni waathiriwa wa sera za kigeni za Marekani. Simulizi ya vyombo vya habari inasema: Magaidi na maadui wa demokrasia wanaangamizwa.
3. Ukweli wa nyanjani unaeleza kuwa uingiliaji kati wa Marekani unaangamiza uchumi na amani ya nchi mbalimbali, lakini simulizi za vyombo vya habari zinasema: Marekani inajenga jamii huru, iliyoendelea na ya kisasa.
4. Ukweli na uhakika wa mambo unasema: Kuna mapambano ya watu dhidi ya uvamizi au ukandamizaji, lakini simulizi ya vyombo vya habari vya Marekani na washirika zinapindua ukweli huo na kusema: Muqawama na mapambano ya aina yoyote “ukatili,” “uasi,” au “misimamo mikali.” ******
Naam, mpenzi msikilizaji! Katika karne ya 21, silaha kuu ya Marekani si mabomu, dunduki na mizinga, bali ni simulizi za vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tasnia ya filamu. Marekani imeunda “mizinga” ya simulizi. Filamu na vipindi vya televisheni ni bunduki zisizo na risasi ambazo hushinda tamaduni kimya kimya, na asteaste.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, dunia imebadilika. Vyombo huru vya habari, mitandao ya kijamii, waandishi huru wa habari, watengenezaji wa filamu za matukio ya kweli (ducumentary), na hata watu wa kawaida wenye simu janja, sasa wanatoa changamoto na kukadhibisha simulizi ya Marekani. Kwa mara ya kwanza, Marekani inapoteza ukiritimba wake kwenye medani ya simulizi kuhusu matukio mbalimbali ya dunia. Harakati za wananchi huko Magharibi, maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu, harakati ya BDS, mwamko wa Afrika, matukio ya Amerika Kusini na muuqawama wa watu wa Asia Magharibi, yote haya yameathiri vibaya “ufalme” na udhibiti wa vyombo vya habari wa Marekani. Ulimwengu si hadhira tena ilnayoketi tu na kulishwa matango pori na simulizi za Marekani.
Marekani imetumia miaka mingi kubadilisha taswira yake kupitia zana kama vile Millennium Media. Lakini leo, ulimwengu unaona nyuma ya pazia la simulizi ya Marekani. Huenda Marekani bado ina nguvu, lakini sio tena msimuliaji pekee duniani. Watu, sasa wameingia katika medani ya simulizi kwa nguvu kubwa. Huu ni mwanzo wa zama mpya katika historia ya vyombo vya habari na mapambano ya kitamaduni.
Sasa, sura halisi ya madola ya kibeberu imefichuka. Barakoa ya taswira ya Marekani kama “mwokozi” imeanguka chini, na ulimwengu umegundua kuwa, nyuma ya kaulimbiu za kutetea uhuru na demokrasia, kumefichwa maslahi na shinikizo ya kisiasa.