MAENDELEO ya afya ya msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya na mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule ‘Professor Jay’, yameimarika kwa kiasi kikubwa, huku ikitabiriwa kuwa atarejea rasmi katika majukumu yake ifikapo mwaka 2026.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kutimiza umri wa miaka 50 wa Professor Jay,Mama Lisa amesema kuimarika kwa afya ya msanii huyo ni matokeo ya rehema za Mwenyezi Mungu na ustahimilivu mkubwa katika kipindi cha matibabu.
“Tunapomshukuru Mungu kwa mume wangu kutimiza miaka 50, tunaziona rehema zake kwa namna afya yake ilivyotengemaa. Kulikuwa na nyakati ngumu zilizojaa maumivu na majaribu, lakini leo hii ni mzima, imara na ana afya njema,” alisema. SOMA: Prof Jay: DM yangu ina maombi mengi mno
Aidha, alibainisha kuwa kutokana na hatua hiyo kubwa ya kurejea kwa afya yake, kuna matumaini ya kumuona msanii huyo akirejea kulitumikia taifa kupitia sanaa na shughuli za kijamii kuanzia mwaka 2026, akiwa na ari mpya.
Professor Jay, ambaye mchango wake katika tasnia ya muziki na uongozi wa umma unatambulika kitaifa, amekuwa nje ya majukumu yake ya kawaida kwa muda mrefu kutokana na matibabu, hali iliyowahusisha viongozi wa kitaifa na wadau mbalimbali wa sanaa kumuombea na kumuunga mkono.
