
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma, imeridhia maombi ya Chama cha ACT–Wazalendo ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama kupinga uteuzi wa wabunge wa viti maalumu uliofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Uamuzi huo umetokana na shauri lililofunguliwa na Wadhamini Waliosajiliwa wa ACT–Wazalendo dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiiomba mahakama kutoa kibali cha kufungua shauri la mapitio ili kupinga uteuzi huo.
Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, INEC ilitangaza uteuzi wa wabunge 115 wa viti maalumu na Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipata wabunge 113 na Chama cha Chaumma wabunge wawili.
ACT–Wazalendo ambacho kilishiriki uchaguzi huo bila mgombea urais, hakikupata mbunge yeyote wa viti maalumu.
Kufuatia tangazo hilo lililotolewa kwa umma Novemba 7, 2025, ACT–Wazalendo kiliwasilisha maombi ya kibali cha kufungua shauri la kupinga uteuzi huo.
Katika shauri la madai mchanganyiko namba 28632/2025, chama hicho kiliomba mahakama itoe kibali cha kufungua shauri la mapitio, itengue uamuzi wa INEC wa kuwateua wabunge hao bila kuwajumuisha wanachama wake na kuilazimisha INEC kufanya uteuzi kwa mujibu wa sheria, wakiwamo wanachama wa ACT–Wazalendo.
Pia, wameiomba Mahakama itamke kuwa kifungu cha 112 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 hakikuhusika katika mazingira ya shauri hilo.
Katika uamuzi wake uliotolewa leo Jumanne, Desemba 30, 2025, Jaji Sedekia Kisanya aliyesikiliza shauri hilo, ameridhia maombi ya ACT–Wazalendo baada ya kubaini mwombaji amekidhi vigezo vyote vya kisheria vinavyohitajika kupewa kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kimahakama.
Shauri hilo liliungwa mkono na kiapo cha Mhongwa Ruhwanya, mdhamini wa ACT–Wazalendo pamoja na Taarifa ya Ukweli, vilivyoeleza historia na misingi ya kisheria ya maombi hayo.
Kwa mujibu wa kiapo hicho, ACT–Wazalendo kilishiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kikitarajia kupata angalau asilimia tano ya kura zote za wabunge, kiliwasilisha kwa INEC orodha ya awali ya wanachama wanawake waliopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalumu.
Chama hicho kimedai baada ya uchaguzi kilipata kura 2,222,162 katika majimbo 181, sawa na asilimia 6.77 ya kura zote zilizopigwa, hivyo kutimiza kigezo cha kisheria cha kupata wabunge wa viti maalumu.
Hata hivyo, kinadai INEC ilitangaza uteuzi wa wabunge 115 bila kuthibitisha rasmi idadi ya kura za chama hicho na bila kumteua hata mbunge mmoja kutoka ACT–Wazalendo.
Awali, INEC na AG waliwasilisha pingamizi la awali wakidai maombi hayo hayakuwa na sifa na kwamba, Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Pingamizi hilo na maombi ya msingi yalisikilizwa kwa pamoja kwa njia ya maandishi.
Hoja za mwombaji ziliwasilishwa na wakili John Seka, ambaye pia alijibu pingamizi la awali na kueleza namna mteja wake alivyokidhi matakwa ya kisheria ya kupewa kibali cha kufungua shauri.
Kwa upande wa wajibu maombi, hoja zimewasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Stanley Kalokola aliyefafanua misingi ya pingamizi hilo na kujibu hoja za maombi ya kibali.
Katika uamuzi wake, Jaji Kisanya ametupilia mbali pingamizi la awali baada ya kubaini kuwa halina mashiko.
Kuhusu shauri la msingi, amesema mwombaji amekidhi vigezo vya kuwepo kwa mgogoro unaobishaniwa, kuwasilisha maombi ndani ya muda wa kisheria wa miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi unaopingwa na kuwa na maslahi ya moja kwa moja katika shauri hilo.
Amesema ACT–Wazalendo kina maslahi katika uamuzi wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu.
“Kwa sababu hizo, ninaridhika kuwa maombi yana msingi. Kibali cha kuomba mapitio ya kimahakama kinatolewa,” amesema Jaji Kisanya.