Pwani. Tanzania imerekodi ongezeko la mitaji hadi kufikia Sh26.95 trilioni katika mwaka 2025 huku China, Nchi za Jumuiya za Kiarabu, Cayman Islands, Uingereza na India zikiongoza kwa kuchangamkia fursa hizo.

Ukuaji wa mitaji iliyowekezwa unatokana na ongezeko la miradi iliyosajiliwa iliyofikia 915 mwaka huu kutoka miradi 901 iliyokuwapo mwaka jana.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa nchi Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika hafla ya kukabidhi hati kwa wawekezaji sita katika eneo la Bagamoyo mkoni Pwani tukio lililoenda sambamba na utoaji wa takwimu za uwekezaji mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo amesema ongezeko la uwekezaji huo inatokana na ukuaji wa shughuli za kibiashara nchini. 

Miradi hiyo imeelekezwa katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, ujenzi, nishati, usafirishaji, kilimo-biashara na huduma na inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 161,678.

Kwa mujibu wa takwimu za uwekezaji, China imeshika namba moja baada ya kuwekeza Sh7.68 trilioni na kuzalisha ajira 81,664 sawa  zaidi ya nusu ya ajira zote zilizotarajiwa kutokana na uwekezaji wa kigeni. 

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ilikiwa nafasi ya pili ambayo iliwekeza Sh 2.172 trilioni ambayo itazalisha ajira 8,426. 

Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akimkabidhi hati ya ardhi mwekezaji mmoja kati ya sita waliopewa maeneo Bagamoyo mkoani Pwani.

“Uingereza imeshika nafasi ya tatu kwa uwekezaji wa Sh2.028 trilioni,Cayman Islands iliwekeza Sh972.359 bilioni na India ikiwa nafasi ya tano kwa kuwekeza Sh809.38 bilioni,” amesema Profesa Mkumbo.

“Uwekezaji huu umejikita zaidi katika miradi ya viwanda, ujenzi wa miundombinu, nishati na uzalishaji wa bidhaa kwa soko la ndani na nje,” amesema.

“Miradi hiyo ipo katika sekta mbalimbali
zikiwemo viwanda (manufacturing), ujenzi wa majengo, na usafirishaji. Katika umiliki wa miradi hiyo wageni ni 182, miradi 284 inamilikiwa na watanzania, na miradi 449 inamilikiwa na wageni,” amesema Profesa Mkumbo.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021 miradi ya uwekezaji iliyokuwa imesajiliwa ilikuwa 252, ambayo iliongezeka hadi kufikia 293 (2022), miradi 526 mwaka 2023 na 901 mwaka jana.

Miradi hiyo ilikuwa na thamani ya Sh9.32 trilioni mwaka 2021, Sh11.15 trlioni mwaka 2022, Sh14.08 trilioni mwaka 2023 na Sh22.91 trilioni.

Kufuatia ongezeko hilo, Tanzania imeingia katika orodha ya nchi kumi bora za uwekezaji Barani Afrika, baada ya kupanda nafasi
tatu kutoka nafasi ya 12 mwaka jana hadi nafasi ya 9 kwa mwaka 2025 kwa mujibu wa  kulingana na Ripoti ya RMB (2025). 

“Mafanikio haya pia yameifanya T anzania
kuwa Nchi ya Kwanza kwa mazingira bora ya uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki,” amesema Profesa Mkumbo.

Kwa upande wa mgawanyo wa uwekezaji kwa mikoa, Dar es Salaam inaongoza ikiwa na miradi 334 inayozalisha ajira 33,707.

“ Jiji hili limeendelea kuwa kitovu cha biashara na huduma, likivutia makampuni ya ndani na ya kimataifa kutokana na miundombinu yake, masoko na upatikanaji wa huduma za kifedha,” amesema Profesa Mkumbo.

Mkoa wa Pwani umeshika namba mbili ikiwa na miradi 208, Arusha ilisajili miradi 67, Dodoma ikiwa na miradi 37 na Mwanza 35.

“Usajili huu wa miradi kwa wingi kwa mwaka 2025 ni ishara kuwa Tanzania imeendelea kuwa sehemu salama ya uwekezaji katika Ukanda wa Afrika kupitia uwepo wa
taasisi imara za kufanikisha uwekezaji, kuwa na Sheria na Sera zinazotabirika za kifedha na
kiuwekezaji, kuwepo kwa fursa nyingi za kuwekeza, utulivu wa kisiasa na kuwa na vivuti vya kikodi na visivyo vya kikodi,” amesema.

Ili kuhakikisha uwekezaji unaendelea kuongezeka zaidi, serikali imeanzisha Jukwaa la Uwekezaji la Kitaifa kwa ajili
ya kukutana na wawekezaji na kufanya tathmini ya uwekezaji nchi. 

“Kuanzia Januari 2026, Tiseza itakuwa na jukumu la kuratibu jukwaa hili ambalo litahusisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Fedha, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Muungano na Mazingira na taasisi ili kukutana na wawekezaji kwa dhumuni la kufanya tathmini ya uwekezaji nchini, kusikilizachangamoto, kupokea maoni, na kuyafanyia kazi,” amesema Profesa Mkumbo.

Akizungumzia utoaji wa maenso kwa wawekezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri amesema mikataba iliyosainiwa leo ni matokeo ya mchakato wa kina ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi na taasisi za kitaalamu. 

“Kupitia mikataba hii, wawekezaji wanapatiwa maeneo rasmi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao, huku Tiseza ikihakikisha kuwa masharti yote yanazingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi yetu pamoja na kulinda maslahi mapana ya Taifa,” amesema.

Amesema Tiseza imekamilisha taratibu za ndani za upatikanaji wa ardhi na maandalizi ya mikataba na takribani makampuni sita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ndani ya Eneo Maalum la Uchumi la Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC SEZ).

 Miradi hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa viwandani, kuongeza mauzo ya nje, uhamishaji wa teknolojia na kukuza ajira hususan kwa vijana pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii Bagamoyo na maeneo jirani.

Kampuni ya kwanza iliyopewa eneno ni Canary Industries Limited ambayo itawekeza Sh1 bilioni kuanzisha kiwanda cha kisasa cha vifungashio vya chakula (PET na PP) katika eneo la ekari 1 Bagamoyo. 

Mradi utaongeza thamani ya uzalishaji wa ndani, kupunguza uagizaji kutoka nje, kusaidia wajasiriamali wadogo na kukuza mauzo ya nje hususan Rwanda na DRC.

Kampuni ya pili ni Grosso Engineering and Fabricators Limited itakayowekeza Sh12.8 bilioni ikitarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 100 za kudumu na ajira 200 za muda. Mradi utaimarisha sekta ya uhandisi, kupunguza uagizaji wa mashine kutoka nje na kusaidia ajenda ya ajira kwa vijana na maendeleo ya viwanda.

Akiitaja kampuni nyingine Teri amesema ni Jaribu Cashwes Produaction Limited itakayokuwa ikichakata mazao ya kilimo. 

Mradi huo utakuwa na thamani ya Sh12.32 bilioni kwa ajili ya kuongeza thamani ya korosho, kahawa na viungo kwa masoko ya kimataifa. Utazalisha ajira zaidi ya 140 za kudumu na za muda, nyingi zikiwa za vijana.

“Kampuni Novara Global Steel Limited itawekeza Sh19.71 bilioni katika uzalishaji wa bidhaa za chuma kwa soko la ndani na nje. Takribani asilimia 80 ya uzalishaji inalenga mauzo ya nje, kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuleta ajira zaidi ya 100 kwa Watanzania,” amesema Teri.

Kampuni nyingine ni Shah Steel Global iliyopanga kuanzisha kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa Ferro Alloys kwa uwekezaji wa awali Sh12.3 bilioni Mradi unatoarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 200 na kuingiza kati ya Sh79.8 bilioni hadi Sh105.959, bilioni kwa mwaka kupitia mauzo ya nje, sambamba na uhamishaji wa teknolojia na ujuzi kwa vijana wa Kitanzania.

“MCGA Ato Limited wao wataunganisha magari uwekezaji wa takribani USD 50 milioni. Kiwanda kitaunganisha magari ya aina mbalimbali kwa soko la ndani na la kikanda,” 

“Mradi unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 500 hadi 1,000 na zaidi ya ajira 3,500 zisizo za moja kwa moja, pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta ya magari nchini, kupunguza uagizaji wa magari kutoka nje na kuongeza mapato ya Serikali,” amesema.

Teri amesema Utekelezaji wa miradi hii unatarajiwa kuleta manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, kukuza minyororo ya thamani ya ndani, kuongeza mapato ya Serikali, na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Bagamoyo na maeneo ya jirani. 

“Aidha, uwekezaji huu utaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *