Maelfu ya wananchi wa Somalia wameendelea kumiminika mabarabarani katika miji mbali mbali ya nchi hiyo, kupinga na kulaani uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kulitambua eneo la Somaliland la kaskazini mwa nchi kama taifa huru.

Huko Baaydhabo, mji ulioko katika jimbo la Kusini Magharibi, maelfu ya watu jana Jumanne waliingia mitaani kupinga hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland,wakiitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa uhuru wa Somalia. Waandamanaji walipeperusha bendera za Somalia na kupiga nara za kuilaani Israel.

Maandamano mwengine yalifanyika huko Hobyo, katika eneo la kati la Mudug, ambapo maelfu waliandamana na kulaani kitendo cha kutambuliwa Somaliland kama nchi huru, wakisema uamuzi huo ni tishio kwa umoja wa ardhi ya Somalia. Huko Xudur, makao makuu ya mkoa wa Bakool, washiriki wa maandamano hayo waliitaja hatua ya Israel kuwa uingiliaji wa wazi wa uhuru wa Somalia na mamlaka ya kitaifa.

Umati mkubwa wa watu huko Guriceel, jimbo la Galmudug, ulibeba mabango yenye jumbe za kupinga kutambuliwa eneo la Somaliland ambalo lilijitangazia uhuru wake mwaka 1991, huku waandamanaji huko Laascaanood, makao makuu ya jibo la Kaskazini Mashariki, wakifanya maandamano kama hayo kwa ushiriki mkubwa wa watu.

Siku ya Jumapili, mamia ya Wasomali walifanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu kupinga kitendo hicho cha Wazayuni cha kujaribu kuigawanya vipande vipande Somalia. Walisema jamii ya kimataifa haipaswi kukaa kimya mkabala wa uamuzi huo batili wa utawala wa Kizayuni.

Abdi Ismail, mmoja wa waandamanaji amenukuliwa na wanahabari akisema, “Hakuna ardhi ya Somalia ambayo itakabidhiwa kwa Israel au dola lolote lile.Somalia ni moja na itabaki kuwa moja, Wasomali wako tayari kufanya chochote kwa ajili ya kuilinda nchi yao. Uamuzi wa Israel haukubaliki na ni shambulio la wazi dhidi ya uhuru wa Somalia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *