Mataifa na asasi mbalimbali za Kiafrika, Kiarabu na Kiislamu zimepinga vikali hatua ya utawala vamizi wa Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland’, ambalo limejitenga na Somalia, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili imekabiliwa na radiamali kali ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa.
Upinzani huo ni mkubwa kiasi kwamba, umeitambua hatua ya Israel kuwa, inakiuka wazi sheria za kimataifa na ni tishio kubwa dhidi ya usalama na uthabiti wa eneo la Pembe ya Afrika.
Kijiografia Somaliland iko kaskazini mwa Somalia mashariki mwa bara la Afrika, kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden. Eneo hilo linapakana na Djibouti kwa upande wa kaskazini magharibi na Ethiopia kwa upande wa kusini magharibi huku likipakana na Somalia kwa upande wa mashariki.
Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa tukiachana na hatua ya hivi majuzi ya utawala ghasibu wa Israel. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.
Somalia inasisitiza kuwa, Somaliland ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia.
Mwishoni mwa mwaka 2024, Kanali ya Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar iliripoti kwamba Somaliland ilikuwa tayari kujadili kuwapokea wakazi wa Gaza ikiwa Israel ingetambua uhuru wa eneo hilo. Uchaguzi wa rais katika eneo la Somaliland ulifanyika Novemba 2024, na Abdirahman Mohamed Abdullahi, kiongozi wa chama cha upinzani aliibuka mshindi katika uchaguzi huo. Wagombea wote wawili katika uchaguzi huo waliahidi kuboresha hali ya kiuchumi na kuchukua hatu kuhakikisha kwamba, uhuru wa Somaliland unatambuliwa kimataifa.
Upinzani mkubwa wa nchi za Kiarabu na Kiislamu dhidi ya hatua ya Israel ya kulitambua rasmi eneo la ‘Somaliland, kama taifa huru na lenye mamlaka kamili unatokana na sababu za kisheria, kisiasa na kiusalama.
Sababu ya kwanza na ya msingi zaidi ni kwamba, hatua hii inakinzana na kanuni zilizowekwa za sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kanuni za uhuru na umoja wa ardhi ya mataifa.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Jumuiya ya Kiarabu na serikali mbalimbali za kikanda zimesisitiza katika taarifa za pamoja kwamba “Somaliland” ni sehemu muhimu ya Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia na kwamba kutambuliwa kama eneo huru na lenye mamlaka kamili ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.
Serikali ya Shirikisho ya Somalia imeitafsiri hatua hiyo ya Israel kama “shambulio la makusudi dhidi ya uhuru wake na umoja wa ardhi yake” na kuonya kwamba, hatua kama hiyo inaweza kudhoofisha utulivu wa ndani na mapambano dhidi ya ugaidi nchini Somalia.
Kufuatia tukio hilo, wimbi la harakati za kidiplomasia lilianza kutoka Mogadishu, likiungwa mkono na wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu na nchi za Afrika Mashariki, ili kuimarisha upinzani dhidi ya hatua yoyote ya kupigania kujitenga. Umoja wa Afrika pia umesisitiza kufungamana kwake na umoja wa ardhi ya Somalia na kutotambua vitendo vyovyote vya kupigania kujitenga.
Sababu ya pili ya upinzani huu ni wasiwasi wa kijiopolitiki kuhusu athari za hatua hii katika Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu. Somaliland iko kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Aden na karibu na Lango Bahari la kimkakati la Bab al-Mandab; njia muhimu kwa biashara ya kimataifa na usafirishaji wa nishati. Nchi za Kiarabu na Kiislamu zimeonya kwamba, kufungua mlango wa kutambua maeneo yaliyotangaza kujitenga katika eneo hilo kutahatarisha na kuyumbisha utulivu, sambamba na kuongeza ushindani wa kijeshi na usalama, na hivyo kushadidisha hatari za baharini.
Sababu ya tatu ya upinzani huu ni hofu ya kuuanzisha ‘ada mbaya’ ya kujitenga katika sehemu zingine za dunia. Taarifa za pamoja za nchi za Kiislamu zinasema kwamba, kuunga mkono mamlaka ya sehemu za eneo la nchi huru kunaunda nidhamu na ada mbaya na husababisha kudhoofika kwa utaratibu wa kisheria wa kimataifa, nidhamu inayotegemea kuheshimu mipaka ya kimataifa na kuepuka kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine.
Pamoja na sababu hizi, pia kuna wasiwasi wa kibinadamu na kisiasa: Baadhi ya nchi zimekataa kabisa kuunganisha hatua hii na mipango tarajiwa ya kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina kutoka Gaza hadi nchi za kigeni. Wanaona hatua hii haikubaliki katika muundo na asili yake, kwani wanaliona jaribio lolote la kulazimisha uhamiaji ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na tishio kwa utulivu wa kikanda.
Lakini swali muhimu linalojitokeza katika muktadha huu ni kwamba, kuna malengo gani nyuma ya pazia ya utawala wa Israel kwa hatua hii isiyo ya kawaida katika uga wa kimataifa?

Mojawapo ya malengo haya ni kupata nafasi ya kijiografia katika Pembe ya Afrika na kuongeza udhibiti wa taarifa katika Bahari Nyekundu, Ghuba ya Aden, na Lango Bahari la Bab al-Mandab. Nafasi ya kijiografia ya Somaliland inatoa fursa ya kufuatilia nyendo za biashara ya nishati, mawasiliano ya baharini ya Yemen, na njia za meli. Ukweli wa mambo ni kuwa, uamuzi wa Tel Aviv unaendana na miradi mipana ya kupenya bandari muhimu, kuimarisha mifumo ya usikilizaji na mawasiliano, na kuanzisha maingiliano ya kiusalama na baadhi ya watendaji wa kikanda.
Lengo jingine ni kujaribu kuongeza na kupanua mradi wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel kwa mtindo wa Makubaliano ya Abraham, ingawa katika mfumo ambao bado haujatambuliwa kimataifa; kitendo ambacho kinaweza kuipa Tel Aviv faida za kinembo na uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kilimo, afya, na teknolojia, licha ya kuwa unaambatana na gharama kubwa za kisheria na usalama.
Lengo la tatu ni kuwa na ushawishi katika milingano ya kikanda na kupunguza ushawishi wa washindani wake. Baadhi ya ripoti zinaiona hatua hii kama sehemu ya wenzo mpana wa kusimamia ushindani katika Bahari Nyekundu na maeneo ya kando kando, ikiwa ni pamoja na kuzingira au kudhibiti uwezo wa uendeshaji wa pande zinazopingana na Israel na washirika wake. Hata hivyo, upinzani wa pamoja wa taasisi na nchi za Kiafrika, Kiarabu, na Kiislamu unaonyesha kwamba si Somalia pekee, bali pia taasisi na serikali mbalimbali za kikanda zimetathmini hatua hii kama ya kuingilia kati masuala ya ndani ya mataifa mengi na ni ya kichochezi.
Kwa muktadha huo, inaweza kusemwa kwamba, radiamali na majibu yaliyoratibiwa ya asasi na nchi za Kiafrika, Kiarabu, na Kiislamu inaonyesha kwamba, uamuzi huu wa utawala wa Kizayuniwa Israel sio tu kwamba hauna uhalali, bali pia utaambatana na gharama kubwa za kiusalama na kisheria kwa eneo hilo na kwingineko.