Leo ni Jumatano tarehe 10 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe 31 Disemba 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake.

Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake.

Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua.

Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar. 

Tarehe 10 Rajab miaka 1252 iliyopita, alizaliwa Imam Muhammad Taqi mmoja wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad SAW katika mji mtakatifu wa Madina. 

Imam Taqi Al-Jawad (as) alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha (as). Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya ‘Jawad’ yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa.

Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura.

Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: “Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui.”   

Tarehe 31 Disemba miaka 511 iliyopita Andreas Vesalius, daktari na mpasuaji maarufu wa Ubelgiji, alizaliwa huko Brussels, mji mkuu wa nchi hiyo. 

Umaarufu wake unatokana na juhudi zake za kuelewa kazi ya viungo mbalimbali vya mwili kupitia upasuaji wa viungo hivyo. Kwa sababu hii, Vesalius ameitwa baba wa sayansi ya anatomia, na kitabu chake kiitwacho “Kiwanda cha Mwili wa Binadamu” (The Factory of the Human Body) pia kinazungumzia maudhuui hii. aliaga dunia mwaka 1564.     

Katika siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, yaani tarehe 31 Disemba mwaka 1827 kibiriti kilivumbuliwa na John Walker mtaalamu wa madawa wa Uingereza.

Hata hivyo awali, mbali na kibiriti cha Walker kuwaka kwa taabu na mashaka kilikuwa pia na hatari kwa watumiaji wake. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana wataalamu wengine wakafanya jitihada za kukikamilisha kibiriti hicho.

Hatimaye mwaka 1855 mtaalamu mmoja wa Kiswedeni alifanikiwa kutengeneza kibiriti kama hiki kinachotumiwa leo hii baada ya kufanya majaribio na utafiti wa muda mrefu.   ****

Miaka 150 iliyopita katika siku kama ya leo Arthur Christensen mtaalamu wa masuala ya Mashariki alizaliwa huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark.

Christensen alionyesha hamu kubwa ya kujifunza masuala ya Mashariki hususan historia ya Iran na mwishoni mwa masomo yake, alifanya utafiti kuhusu historia ya fasihi ya Irani.

Arthur Christensen aliweza kujifunza vyema lugha ya Kifarsi. Mojawapo ya vitabu vyake muhimu ni kile alichokipa jina la “Iran katika Zama za Wasasani.” Christensen aliaga dunia mwaka 1945.   

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita iliundwa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait kwa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Shia na wafuasi wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kote duniani, kujenga uhusiano baina yao, kunyanyua juu kiwango cha shule za kidini, kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza baina ya wafusi wa Ahlul Bait na madhehebu nyingine za Kiislamu na kadhalika.   

Tarehe 31 Disemba mwaka 1994 yaani siku kama hii ya leo miaka 31 iliyopita, Idhaa ya Kiswahili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliaanzishwa kwa shabaha ya kufikisha sauti na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wazungumzaji wa lugha hiyo.

Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran yanahusu masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika. Kwa sasa unaweza kuyasikiliza matangazo yetu kwa njia ya moja kwa moja na kupitia hifadhi ya matangazo wakati wowote. Unaweza pia kuyapata matangazo ya Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran kupitia simu ya mkononi bila ya kutoa malipo yoyote isipokuwa gharama zako za kawaida za Intaneti kupitia njia ya kupakua aplikesheni ya matangazo yetu ya IRIB World Service.

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Rais Boris Yeltsin wa Russia aliondoka madarakani na nafasi yake ikachukuliwa na Vladimir Putin.

Kipindi fulani Yeltsin alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti. Boris Yeltsin alichaguliwa kuwa Rais wa Russia Januari mwaka 1991 na alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi. Hata baada ya kusambaratika Umoja wa Sovieti mwishoni mwa mwaka 1991, aliendelea kuwa Rais wa Russia akitumai kwamba, kwa kutumia misaada ya kifedha ya Magharibi angeweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi yake ya kiuchumi.

Kinyume na matarajio yake, viongozi wa madola ya Magharibi hawakutekeleza ahadi zao, hali iliyopelekea siasa za Rais Boris Yeltsin kushindwa.

Kushambuliwa kijeshi eneo lililotangaza kujitawala la Chechnia na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo na majeshi ya Russia, ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika kipindi cha utawala wa Boris Yeltsin nchini Russia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *