
Tume ya uchaguzi ya Guinea Conakry ilitangaza jioni ya jana Jumanne kwamba kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Mamadi Doumbouya, ameshinda kwa kishindo kwa kupata asilimia 86.72 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais.
Uchaguzi huo uliofanyika Jumapilii iliyopita ulikuwa kilele cha kipindi cha mpito cha miaka minne baada ya mapinduzi yaliyomfikisha madarakani Mamadi Doumbouya katika taifa hilo la Afrika lenye utajiri wa bauxite na madini ya chuma.
Mkuu wa Tume Kuu ya Uchaguzi ya Gunea Conakry, Djenabo Toure, amesema asilimia 80.95% ya waliojiandikisha kupiga kura wameshiriki katika zoezi hilo.
Kiongozi wa chama cha Democratic Front of Guinea (Frondg), Abdoulaye Yero Balde, ameshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 6.59 ya kura.
Mapema jana Jumanne, wagombea wanne kati ya wanane walioshindana na kiongozi wa kijeshi wa Guinea walikubali kushindwa na kumpongeza Doumbouya kwa kupata ushindi katika raundi ya kwanza ya uchaguzi.
Mahakama Kuu ya Gunea Konacry inatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ndani ya siku nane zijazo.
Waangalizi huru wameeleza kuwa upigaji kura ulifanyika katika mazingira tulivu na bila vurugu.
Uchaguzi wa urais nchini Guinea Conakry umefanyika kufuatia kura ya maoni ya katiba ya mwezi Septemba mwaka huu ambayo iliandaa mazingira ya kurejea utawala wa kiraia, na wakati huo huo kushiriki katika kinyang’anyiro hicho Rais wa Serikali Mpito, Jenerali Mamadi Doumbouya, mwenye umri wa miaka 41.
Doumbouya ambaye ni Kamanda wa Vikosi Malaumu mwenye uzoefu wa majukumu nje ya nchi, aliongoza mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu Septemba 5 mwaka 2021 na kumpindua Rais wa wakati huo, Alpha Conde.