
Polisi nchini Ghana wamemkamata mwanamume
aliyenaswa kwenye video ya mtandaoni akifyatua bunduki wakati wa tamasha la
muziki mjini Accra.
Mshukiwa huyo, aliyetambulika kama
Abubakari Sadick, maarufu kama “Cyborg”, alitoa bunduki hiyo wakati
wa mkutano na mwanamuziki wa Nigeria Asake, kinyume na Sheria ya Silaha za Moto
na Sheria ya Utaratibu wa Umma.
Alikamatwa
na Timu ya Uchunguzi wa Mtandao (Cyber Vetting Team)
katika Makao Makuu ya CID baada ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kutaka
akamatwe kwa kutoa silaha hiyo kiholela kwenye hafla ya hadhara.
“Kikosi cha Uchunguzi wa Mtandaoni katika
Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) kimemkamata mshukiwa
aliyeonekana kwenye video akionyesha bunduki ya hali ya juu kwenye tamasha la
AfroFuture lililofanyika katika Uwanja wa El-Wak, Accra, tarehe 28 Desemba
2025.”
“Kwa sasa mshukiwa yuko chini ya ulinzi wa polisi, akisaidia katika
uchunguzi, na atafikishwa mahakama kujibu haki,” Inspekta Mkuu Brigitte
Babanawo alisema katika taarifa.
Silaha iliyoonekana mtandaoni,
iliyotambuliwa kama bunduki aina ya Derya MK-12, imechukuliwa kutoka kwa
mshukiwa kama ushahidi.
Polisi nchini Ghana pia wametoa tahadhari kwa
umma juu ya matumizi mabaya ya silaha, wakisisitiza kuwa kumiliki silaha
iliyosajiliwa hakumpatii mmiliki uhuru wa kuitumia kiholela.