k

Chanzo cha picha, Joe Raedle/Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Urusi, Marekani na Ukraine zinasema makubaliano ya kukomesha vita vya karibu miaka minne yanakaribia, lakini kwa maneno ya Rais Donald Trump, “kuna suala moja au mawili ambayo ni magumu sana” yamebaki.

Masuala mawili magumu zaidi katika mpango wa Washington wa vipengele 20 yanahusu mipaka na hatima ya kiwanda kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya, ambacho kwa sasa kinakaliwa na Urusi.

Kremlin inakubaliana na Trump kwamba mazungumzo yako “katika hatua ya mwisho,” lakini mambo yanayoweza kukwamisha mazungumzo yanaweza kuhatarisha makubaliano yote.

Pia unaweza kusoma

Mipaka ya Ukraine

Vladimir Putin hajaachana madai yake juu ya kutaka kuishikilia Donbas yote, mji wa viwanda wa Ukraine.

Vikosi vya Urusi vinashikilia sehemu kubwa ya eneo la Luhansk mashariki lakini inashikilia 75% ya Donetsk, na Putin anataka kushikilia eneo lote, ikiwa ni pamoja na miji iliyobaki ya Sloviansk na Kramatorsk.

“Hatuwezi kujiondoa tu kwenye maeneo hayo, ni kinyume cha sheria yetu,” anasema Zelensky. “Siyo sheria pekee. Watu wanaishi huko, watu 300,000 … Hatuwezi kuwapoteza.”

Zelensky amekubali vikosi vya Ukraine viondoke kutoka eneo hilo ili kuunda eneo lisilo la kijeshi au eneo huru la kiuchumi linalolindwa na Ukraine, ikiwa Urusi itajiondoa kwa umbali huo huo pia. Na mipaka itasimamiwa na vikosi vya kimataifa.

Ni vigumu kufikiria Putin atakubali lolote kati ya hayo, kwani majenerali wa Urusi wanamwambia wanaliteka eneo la Ukraine kwa kasi sana.

“Ikiwa serikali ya Kyiv haitaki kutatua jambo hili kwa amani, tutatatua matatizo yote yaliyo mbele yetu kwa njia za kijeshi,” amesema Putin.

Pande zote mbili zinaonekana zinakabiliwa na uchovu wa vita. Wachambuzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Vita wanakadiria itavichukua vikosi vya Urusi hadi Agosti 2027 kuteka sehemu iliyobaki ya Donetsk ikiwa wataweza kudumisha kiwango chao cha sasa cha kusonga mbele – ambacho si cha uhakika.

Mapendekezo ya Zelensky pia yatawataka wanajeshi wa Urusi kuondoka katika maeneo mengine ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na eneo la Kharkiv na Sumy kaskazini, Dnipropetrovsk mashariki na Myokolaiv kusini.

Bila ya kupata muafaka kuhusu Donetsk, nafasi ya makubaliano ya amani inaonekana kuwa ngumu.

Mjumbe wa Kremlin, Yuri Ushakov alisema hivi karibuni “inawezekana kabisa kwamba hakutakuwa na wanajeshi wowote [huko Donbas], iwe wa Urusi au wa Ukraine,” ingawa aliweka msimamo kwamba eneo hilo litakuwa sehemu ya Shirikisho la Urusi.

Kiwanda cha nyuklia cha Ukraine

n

Chanzo cha picha, Getty Images

Tangu Machi 2022, Urusi imechukua himaya ya kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya huko Enerhodar, kwenye kingo za mto Dnipro, ingawa kiwanda hicho hakizalishi umeme.

Ili kukifanya kizalishe umeme tena kunahitajika uwekezaji mkubwa, ikiwemo kujenga upya bwawa la maji la Kakhovka lililoharibiwa ambalo lilitumika kutoa maji ya kupoza kiwanda.

Ukraine inaamini eneo hilo pia linapaswa kutotumiwa kijeshi na kugeuzwa kuwa eneo huru la kiuchumi.

Pendekezo la Marekani, kulingana na Zelensky, ni kwamba Marekani isimamie kiwanda hicho kama eneo la pamoja kati ya Urusi na Ukraine.

Kyiv imesema hilo haliwezekani na badala yake Marekani na Ukraine zinaweza kusimamia kwa pamoja 50-50, huku Marekani ikiamua nusu ya umeme iende wapi – kwa kumaanisha Urusi.

Tatizo ni kwamba Urusi haitaki kukiachilia kiwanda hicho na mkuu wa shirika la nyuklia la Rosatom la Urusi, Alexei Likachev amesisitiza kwamba ni Urusi tu – ndio inayoweza kukiendesha na kuhakikisha usalama wake.

Amesema Ukraine inaweza kutumia umeme unaozalishwa na kiwanda hicho katika muktadha wa ushirikiano wa kimataifa.

Kutoaminiana

Wakati Trump aliposema wiki hii kwamba Putin “anataka kuiona Ukraine ikifanikiwa … ikiwa ni pamoja na kusambaza nishati … kwa bei ya chini sana,” ni wazi kuwa Zelensky hakuamini hata neno moja – hamchukulii Putin kama mtu wa kumuamini kuhusu amani.

“Siiamini Urusi… Simwamini Putin, na hataki mafanikio kwa Ukraine,” kiongozi huyo wa Ukraine alisema.

Urusi pia imeonyesha kuwa na imani ndogo na Kyiv – ikivishutumu vikosi vya Ukraine kwa kupeleka ndege zisizo na rubani katika makazi ya Putin katika eneo la Novgorod, ingawa haikutoa ushahidi wowote wa shambulio hilo.

Ukraine inakanusha hilo na inaamini ni kisingizio cha Urusi ili kufanya mashambulizi zaidi kwenye majengo ya serikali huko Kyiv.

Mambo mengine

Kyiv imewaomba viongozi wa Marekani na Ulaya dhamana za usalama ili kuhakikisha inapokea usaidizi kama wa Nato iwapo Urusi itaishambulia zaidi. Ukraine pia inataka kubakisha jeshi lake la wanajeshi 800,000.

Ingawa Marekani na Ulaya zinaweza kusaini makubaliano kuhusu usalama, Urusi haitakubali wanajeshi wa Ulaya kuwepo Ukraine.

Hasara za kifedha kwa Ukraine zinakadiriwa kuwa dola bilioni 800 (£600bn), kwa hivyo suala lingine muhimu ni kiasi gani Urusi itachangia katika hilo.

Marekani inazungumza kuhusu mfuko wa pamoja wa uwekezaji na Ulaya, na Urusi ina mali zenye thamani ya €210bn (£183bn) barani Ulaya ambazo pia zinaweza kutumika, ingawa Moscow hadi sasa imekataa kuruhusu hilo.

Urusi pia inakataa ombi la Ukraine la kujiunga na Nato. Hilo linaweza lisiwe jambo gumu sana kwani hakuna uwezekano wowote wa hilo kutokea.

Uanachama wa Umoja wa Ulaya pia ni kikwazo kinachoweza kutokea, labda si kikwaza kutoka Urusi, bali ni kutokana na foleni ya nchi nyingine za kujiunga na EU. Huenda isitokee hivi karibuni.

Kiongozi huyo wa Ukraine ametaja kura za maoni zinazoonyesha kuwa 87% ya Waukraine wanataka amani, huku 85% wakikataa kujiondoa Donbas.

Kwa hivyo anaamini hakuna uamuzi wowote kuhusu hatima ya Donetsk au mpango mpana wa vipengele 20 unaoweza kufanywa bila kura ya wananchi na usitishaji mapigano wa siku 60 ili kuandaa: “Kura ya maoni kama njia ya kukubali au kutokubali.”

Hili pia ni jambo linaloweza kuzua mvutano kwani Kremlin inasema kusitisha mapigano kwa muda kutaongeza mzozo na kusababisha uadui mpya.

Lakini bila kura kama hiyo, Zelensky anaamini makubaliano hayatakuwa na uhalali wowote, jambo ambalo linaongeza orodha ya masuala magumu yanayopaswa kutatuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *