DAR ES SALAAM; Mwaka 2025 umeacha kumbukumbu nzito kwa Watanzania, ukiwa na mchanganyiko wa matumaini, majonzi na majaribu makubwa.
Miongoni mwa matukio yaliyogusa hisia za wengi ni kupoteza wapendwa, viongozi na wananchi katika ajali na majanga mbalimbali yaliyotikisa nchi kwa kipindi chote cha mwaka.
Tukio kubwa lililotia huzuni zaidi ni ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Juni 30, 2025, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ambapo watu 42 walipoteza maisha.

Kati ya marehemu hao, 31 walikuwa wakisafiri katika basi dogo aina ya Toyota Coaster, wakiwemo wanawake 21 na wanaume 10.
Wengine 11 walikuwa abiria wa basi la Kampuni ya Channel One, wakiwemo wanawake saba na wanaume wanne.
Mapema mwezi huohuo wa Juni, tarehe 8, taifa lilikuwa linaomboleza tena baada ya watu 28 kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa katika ajali ya barabarani jijini Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea baada ya lori lililobeba mzigo wa unga kushindwa kufunga breki na kugonga magari mawili, likiwemo daladala.
Agosti 13, 2025, janga jingine kubwa lilitikisa taifa baada ya sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Nyandolwa, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, mkoani Shinyanga, kuporomoka wakati wa matengenezo.
Tukio hilo, linalodhaniwa kusababishwa na mtikisiko wa ardhi, liliwasomba wafanyakazi na mafundi 25 waliokuwa ndani ya mashimo ya mgodi.
Mwezi Julai nao haukupita bila majonzi, wanafunzi watano wa Shule ya Sekondari Chalangwa, wilayani Chunya, mkoani Mbeya, walifariki dunia katika ajali ya barabarani walipokuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia asubuhi.
Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Safina Coach na kuwaacha wanafunzi wengine tisa wakiwa wamejeruhiwa.
Mwaka ulianza kwa huzuni mwezi Januari 2025, baada ya wanafunzi saba kufariki dunia na 82 kujeruhiwa kufuatia radi kupiga Shule ya Sekondari Businda, eneo la Ushirombo, wilayani Bukombe, mkoani Geita, wakati wa mvua kubwa.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Pasikasi Mulagiri, alisema radi ilipiga kati ya saa 9 na 10 alasiri, wanafunzi wakiwa darasani. Kati ya waliojeruhiwa, 80 walikuwa katika hali nzuri, huku wawili wakiendelea kupatiwa matibabu ya uangalizi maalumu.
Mnamo Aprili 19, 2025, watu saba walifariki dunia na 15 kujeruhiwa baada ya ajali iliyohusisha gari la wagonjwa na chombo cha usafiri cha magurudumu matatu maarufu kama toyo, katika eneo la Luganga, Halmashauri ya Mji wa Mafinga, wilayani Mufindi, mkoani Iringa.
Septemba 14, ajali nyingine ilitokea wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, na kusababisha vifo vya wanafamilia watano wa familia ya Kaggi kutoka Dar es Salaam.
Marehemu walikuwa baba na watoto wake wanne, huku mama yao, Sophia Makange, akinusurika.
Siku mbili baadaye, Septemba 16, masista wanne wa Shirika la Carmelite Missionaries of St Thérèse of the Child Jesus pamoja na dereva wao walifariki dunia baada ya gari lao kugongana uso kwa uso na lori mkoani Mwanza.
Miongoni mwa marehemu ni Sista Nelina Semeoni (60), raia wa Italia na Mkuu Mkuu wa shirika hilo duniani, Sr Lilian Kapongo (55) wa Tabora, Sr Damaris Matheka (51) na Sr Stellamaris Kamene Muthin (48) kutoka Kenya, pamoja na dereva Msonola, mkazi wa Bukumbi.
Taifa pia lilipata pigo kubwa kufuatia kifo cha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, pamoja na dereva wake Muhajir Mohamed Haule, waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani wilayani Bunda, mkoani Mara.