
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mwenzake wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud mjini Istanbul na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo kadhia ya Somaliland.
Mkutano huo wa viongozi wa ngazi za juu wa Somalia na Uturuki umekuja huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kulaaniwa kote duniani kwa kulitambua eneo la Somalia la Somaliland kuwa nchi huru.
Somaliland ilitangaza kujitenga na Somalia zaidi ya miongo miwili iliyopita, lakini imeshindwa kutambuliwa na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Viongozi hao wawili walianza mazungumzo ya pande mbili baada ya sherehe rasmi ya kukaribishwa Rais wa Somalia nchini Uturuki. Majadiliano yalizungumzia hatua za kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Mogadishu na Ankara.
Ajenda nyingine ya mazungumzo hayo ilikuwa ni mapambano yanayoendeshwa na Somalia dhidi ya ugaidi na juhudi za serikali ya Mogadishu za kuhakikisha kuwa umoja na haki ya kujitawala ardhi yote ya Somalia, inalindwa.
Israel ndilo dola la kwanza na pekee lililotangaza kuitambua Somaliland kuwa nchi huru, hatua ya kichokozi ambayo imepelekea kulaaniwa vikali utawala pandikizi wa Israel kuanzia huko Somalia kwenyewe hadi nje yake. Taasisi mbalimbali kuu ukiwemo Umoja wa Mataifa wote wamelaani hatua ya Israel ya kuchochea fitna na kufanya njama dhidi ya haki ya kujitawala ardhi yote ya Somalia.
Hii ni katika hali ambayo maelfu ya wananchi wa Somalia wameendelea kumiminika mabarabarani katika miji mbali mbali ya nchi hiyo, kupinga na kulaani uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kulitambua eneo la Somaliland la kaskazini mwa nchi hiyo kuwa taifa huru. Huko Baaydhabo, mji ulioko katika jimbo la Kusini Magharibi, maelfu ya watu jana Jumanne waliingia mitaani kupinga hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland kama nchi huru, wakiitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa Somalia.