Takriban vijana 41 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na taratibu ‘zisizofaa’ za upashaji tohara nchini Afrika Kusini mwezi Novemba na Desemba mwaka huu unaomalizika wa 2025, mamlaka za nchi hiyo zilitangaza hayo jana Jumanne.

Upashaji tohara, ni sehemu ya utamaduni wa kuingia kwenye ‘utu uzima’ kwa vijana wa kiume ambao hufanywa kila mwaka kwenye jamii mbalimbali barani Afrika, zikiwemo jamii za Afrika Kusini. Miongoni mwao ni jamii za Xhosa, Ndebele, Sotho na Venda.

Vijana wa kiume wakiwa katika ‘skuli za jando’ hufundishwa maadili mema na wajibu wa kitamaduni wanapoingia kwenye utu uzima. Upashaji tohara katika baadhi ya jamii husababisha vifo kwa wanaotahiriwa kila mwaka, na hivyo kuilazimu serikali kuingilia kati kupitia sheria.

Sheria za nchi hiyo zinalazimisha shule za upashaji tohara kusajiliwa na mamlaka, lakini hii haijazuia kuenea kwa shule haramu za unyago ambapo vifo vingi huripotiwa.

Waziri wa Masuala ya Utamaduni wa Afrika Kusini, Velenkosini Hlabisa aliwaambia waandishi wa habari jana Jumanne kwamba, vijana 41 wa kiume waliaga dunia wakati wa kupashwa tohara kwenye msimu wa majira ya joto mwaka huu.

Amesema vifo hivyo vimetokana na uzembe wa baadhi ya taasisi za jando zikiwemo zilizosajiliwa na wazazi, kwa kutozingatia viwango vya usalama na ushauri wa kimatibabu. Hlabisa amesema baadhi ya ushauri ambao mara nyingi wanapewa vijana hao wakiwa jandoni ni kuepuka kunywa maji eti ili wapone haraka.

Jimbo la Eastern Cape limetambuliwa kama sehemu inayoongoza kwa vifo vya vjana wanaopashwa tohara,likisajili jumla ya vifo 21 kufikia sasa. Hlabisa amesema watu zaidi ya 40 wamekamatwa kwa kuendesha taasisi za upashaji tohara ambazo si halali, wakiwemo wazazi ambao walitoa umri usiofaa ili watoto wao wapashwe tohara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *