Rais wa Iran amesisitiza kwamba, jibu la Jamhuri ya Kiislamu kwa uchokozi wowote litakuwa kali na litamfanya adui ajute.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema hayo amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: “Jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uchokozi wowote wa kidhalimu litakuwa kali na la kujutisha.”

Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umetolewa kujibu tishio lililotolewa hivi karibuni na Rais wa Marekani, Donald Trump siku chache zilizopita.

Trump katika mkutano na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu Jumatatu usiku, alijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu kama Marekani ingeruhusu utawala wa Israel kushambulia Iran tena, ambapo alisema: “bila shaka kwa nguvu ya kombora, kwa silaha ya nyuklia, ya haraka sana.”

Donald Trump alitoa bwabwaja hizo mpya alizozitia chumvi akisema: “Ikiwa Iran itaendelea na mpango wake wa makombora, nitaunga mkono kushambuliwa Iran. Ikiwa wataendelea na mpango wao wa nyuklia, tutashambulia mara moja.”

Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimetangaza kuwa, vimejiandaa kikamilifu kutoa majibu makali kwa tishio lolote la usalama wa Jamhuri ya Kiislamu na watu wake na kuonya kwamba, uchokozi wowote mpya wa uadui dhidi ya Iran utakuwa mkali zaidi, angamizi zaidi na wenye madhara makubwa zaidi kuliko huko nyuma.

Aidha Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewaandikia barua mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi jirani na kutaka kulaaniwa waziwazi na kwa uthabiti; bwabwaja na upayukaji wa Trump na Netanyahu akitangaza kwamba, Iran haitosita kutoa jibu kali na la kumjutisha yeyote atakayeshiriki kwenye uchokozi dhidi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *