Mwanamuziki wa Bongofleva, Ben Pol amesema kwa sasa amewekeza nguvu kufanya muziki wa bendi ili kushiriki matamasha mengi ya kimataifa yanayohitaji muziki wenye ladha na kuonyesha uhalisia wa kipaji.

Katika bendi yake inayojulikana kwa jina la Ben Pol and Band, amesema anaimba nyimbo zake na kava za wasanii mbalimbali duniani, huku akifanya sanaa kazi na balozi mbalimbali ukiwemo wa Ufaransa.

“Unapoimba ‘live’ unaonyesha sanaa na kipaji halisi, tofauti na kuweka CD ambao unatumika ufundi mwingi teknolojia ya kompyuta, hivyo huwezi kuona ladha halisi. Mbali na hilo matamasha mengi ya kimataifa yanahitaji bendi na kuimba live,” amesema Ben Pol na kuongeza:

“Ratiba zangu nyingi nafanya kazi na balozi mbalimbali. Tukivuka salama Aprili 2026 nina ratiba ya kwenda Comoro, hivyo bado naendelea kufanya kazi sijakaa… ni vile sijaonyesha sana kazi zangu mtandaoni.”

Akizungumzia mwaka 2025 alivyotumia muda mwingi kurekodi nyimbo na kuzifanyia mazoezi kazi za wengine ili akipanda jukwaani iwe rahisi kupafomu, nyota huyo aliutumia akiwa Ujerumani.

“Japokuwa ulikuwa mwaka ambao nilikaa zaidi Ujerumani kwa ajili ya mambo ya kifamilia, lakini niliutumia kurekodi nyimbo nyingi na mbili niliziachia kama Mpenzi na My Friend zilizopokewa kwa ukubwa zaidi, lakini asilimia kubwa zilizosalia nitazifanyia kazi mwaka 2026,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *