
Serikali ya Sudan Kusini imeagiza raia kuondoka katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi yaliyojihami katika jimbo la Jonglei ili kuepuka kutumika kama ngao wakati wa mapambano, wakati serikali ikiendelea kupambana na makundi hayo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kupitia barua ya msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Lul Ruai Koang, serikali imesema raia wote wanaoishi karibu na kambi za jeshi wanastahili kuondoka mara moja katika maeneo hayo, akiongeza kuwa ni hatua inayolenga kuzuia mauaji zaidi wakati wa operesheni ya kijeshi, ambapo miji ya Nyirol, Uror, na Akobo itaathirika.
Agizo la serikali linajiri siku moja baada ya shambulio la anga kuwaua raia 26 na kuwajeruhi wengine 30 katika soko moja jimboni Nyirol.
Mapigano makali yamekuwa yakishuhudiwa kati ya jeshi la serikali (SSPDF) na lile la upinzani la SPLA–IO tangu mwaka uliopita, baada ya wanajeshi hao wa upinzani kuvamia kambi ya kijeshi ya Waat, jimboni Jonglei.
Mapigano haya yanaendelea wakati mkataba wa Amani uliounda serikali ya umoja wa kitaifa mwaka 2018,kati ya Rais Salva Kiir na hasimu wake wa kisiasa Riek Machar ukionekana kuvunjika, baada ya Machar kufunguliwa kesi ya uhaini, jambo linalotishia kurejesha nchi hiyo kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.