Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Tabora pamoja na Idara ya Mipango Miji kuhakikisha haitoi vibali vya ujenzi katika maeneo ya mabondeni.
Amesisitiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya ujenzi holela katika maeneo korofi, ikiwamo kubomoa majengo yasiyo na vibali pale itakapobidi.
Chacha ametoa maagizo hayo leo Jumatano Desemba 31, 2025 alipofanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua, huku akisema wananchi wanaoishi mabondeni wanakumbwa na athari kubwa ikiwamo nyumba kujaa maji, kubomoka, watu kusombwa na maji na kuhatarisha maisha yao.
Ametaja baadhi ya maeneo hatarishi kuwa ni pamoja na linalozunguka Bwawa la Italia lililopo Kata ya Mapambano, Manispaa ya Tabora, ambalo limepasuka kutokana na mvua kubwa, pamoja na kata za Mwinyi na Malolo.
Wananchi wakiwa katika barabara ambayo imekatika kutokana na bwawa la Italia kujaa kufuatia mvua zinazoendea kunyesha.
Amesema halmashauri inapaswa kutembelea maeneo yote chini ya mamlaka yake ili kuhakikisha matumizi sahihi ya ardhi yanafuatwa.
Amesema maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya makazi yajengwe huku yale ya kilimo yaendelee kutumika kwa shughuli hizo.
“Meya na timu yako msikae ofisini tu. Piteni huko muangalie tatizo lilipo kwa sababu maeneo haya ambayo wananchi wamejenga yalipaswa kutumika kwa kilimo, labda mpunga. Tuchukue tahadhari mapema badala ya kusubiri kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” amesema Chacha.
Kwa upande wake, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Gulam Dewji amesema changamoto kubwa inayoikumba Idara ya Mipango Miji ni ujenzi holela, huku akieleza kuwa baadhi ya maeneo kama Malolo yanahitaji ujenzi imara wenye gharama kubwa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Gulam Dewji akizungumza leo Desemba 31, 2025 mara baada ya kuagizwa kusimamia vibali vya ujenzi
Amesema halmashauri ina mpango wa kutoa notisi ya kuendelezwa kwa majengo imara na kwa watakaoshindwa kufanya hivyo, watapaswa kuwauzia wenye uwezo wayaendeleze.
“Tunalitekeleza hili kwa kusimamia sheria. Naomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tabora iwe karibu nasi, kwa sababu utekelezaji wa sheria huwa na malalamiko na kelele za hapa na pale kuhusu nani yuko sahihi na nani amekiuka utaratibu,” amesema Dewji.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Tabora, Subira Manyama amewashauri wananchi wanaojenga vidaraja binafsi kwa ajili ya biashara au makazi yao, kutumia wataalamu wa Tarura ili kujenga yanayokidhi vigezo.
Meneja wa Tarura wilaya ya Tabora Subira Manyama akielekeza namna bora yakudhibiti athari za maji
Amesema ujenzi usiozingatia utaalamu unasababisha maji kushindwa kupita wakati wa mvua, hivyo kujaa na kuingia kwenye makazi ya watu jambo linaloleta madhara na kuhatarisha maisha.
“Sio kosa mtu kujenga daraja lake mwenyewe, lakini ni muhimu kutumia wataalamu kuepusha madhara wakati wa mvua kubwa kwa sababu maji hujaa haraka na kushindwa kupita,” amesema Manyama.