Iringa. Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Iringa unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh800 milioni unalenga kuondoa msongamano wa wajawazito na kusogeza huduma za afya ya uzazi karibu na wananchi.

 Hatua itakayowanufaisha zaidi ya watu 200,000 ndani na nje ya Manispaa ya Iringa.

 Ujio wa mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo umetajwa kuandika historia kufuatia uwepo wa ujenzi wa wodi mpya ya wazazi huku akina mama 200,000 wakitarajiwa kunufaika na uwekezaji huo.

Wakizungumza na Mwananchi leo Desemba 31, 2025, wananchi wa Manispaa ya Iringa wameeleza matumaini ya kupungua kwa msongamano na kuboreshwa kwa huduma za uzazi katika Hospitali ya Wilaya ya Iringa kufuatia kuanza kwa ujenzi wa wodi mpya ya wazazi.

Mkazi wa Kata ya Mwangata, Rehema Mwakalinga amesema kukamilika kwa wodi hiyo kutasaidia kupunguza hatari kwa kina mama wajawazito.

Godfrey Kalinga amesema mradi huo utapunguza gharama kwa familia zilizokuwa zikilazimika kusafirisha wagonjwa kwenda hospitali nyingine.

Naye Neema Mwenda amesema kuboreshwa kwa mazingira ya uzazi kutahamasisha kina mama wengi zaidi kujifungulia hospitalini badala ya nyumbani.

Mradi huo wa ujenzi wa wodi mpya ya wazazi umeanza baada ya Manispaa ya Iringa kupokea Sh800 milioni kutoka Serikali Kuu kwa lengo la kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada akiwa katika eneo la ujenzi wa wodi ya Wazazi akizungumza na wanahabari leo Desemba 31, 2025. Picha na Christina Thobias

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema ujenzi wa wodi hiyo ni hatua muhimu ya kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya huduma za uzazi katika hospitali hiyo inayohudumia zaidi ya wagonjwa laki mbili kwa mwaka.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Frelimo, Dk Hassan Mtani amesema kukamilika kwa wodi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano uliokuwepo hospitalini hapo.

Dk Mtani amesema mazingira bora ya huduma yataongeza ufanisi wa wahudumu wa afya na kuboresha utoaji wa huduma kwa wajawazito kabla na baada ya kujifungua.

“Mradi huu utakapokamilika utasaidia kuboresha usalama wa mama na mtoto pamoja na kuongeza hadhi ya huduma za uzazi,” amesema Dk Mtani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *