
MLANDEGE FC ni mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi, lakini ilichofanya mechi mbili za hatua ya makundi, yenyewe imeshindwa kujitetea. Inabondwa tu.
Desemba 28, 2025 katika ufunguzi wa michuano hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Mlandege ilichapwa 3-1 na Singida Black Stars.
Leo Desemba 31, 2025, imeufunga mwaka kinyonge baada ya kupigwa bao 1-0 dhidi ya URA kutoka Uganda.
Katika mechi ya leo, Mlandege iliingia tofauti kidogo na ile ya mwanzo kwani benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na kocha mkuu, Hassan Ramadhan na msaidizi wake, Sabri Ramadhan China, liliamua kuwatupa benchi Hashim Suleiman Mussa, Masoud Rashid Juma na Yussuf Suleiman Haji ‘Jussa’, nafasi zao wakianza Abdallah Salum Sio, Said Mussa Said na Jamal Saleh Ali ‘Jaku’.
Licha ya mabadiliko hayo, lakini mapema tu dakika ya sita, Mlandege iliruhusu bao lililofungwa na Amaku Fred aliyetumia mwanya wa kipa, Hamad Ubwa Hamad aliyetoka nje ya boksi na kushindwa kuokoa hatari.
Kuingia kwa bao hilo, ikaifanya mechi kuchangamka zaidi, lakini haikuwa na mabadiliko yoyote ya ubao wa matokeo hadi mwisho Mlandege 0-1 URA.
Mlandege imepoteza mechi zote mbili na kuitoa kwenye mbio za kuwania kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo ikibaki na mechi moja dhidi ya Azam itakayochezwa Januari 2, 2026.
Katika kundi A, Singida ina pointi tatu sawa na URA zote zikicheza mechi moja, huku Azam bado haijashuka dimbani, inacheza usiku huu dhidi ya Singida Black Stars na Mlandege haina kitu ikicheza mechi mbili. Kundi hili timu mbili za juu zinafuzu nusu fainali.