RUVUMA ni mkoa uliowahi kupata changamoto kubwa ya ukosefu wa umeme wa uhakika.
Saa za jioni zilipowadia, giza lilitanda mapema na shughuli za kiuchumi zililazimika ‘kulala.’ Leo, ukiingia mijini au kupenya ndani ya vijiji vya mbali vya mkoa huu, utaona nguzo za umeme zimesimama kama minara ya ushindi na taa za umeme zikipeperusha mwanga unaoonekana kwa mbali; ni mwanga wa matumaini, maarifa na ndoto zinazochipua upya.
Katika muongo mmoja uliopita, nishati ya umeme imegeuka kuwa mhimili mkuu wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Ruvuma. Taa zinawaka nyumbani, katika maduka madogo ya rejareja, vioski vya kuchomea chipsi, gereji, vituo vya afya vilivyojificha pembezoni mwa vijiji na hata kwenye migodi inayolala kilomita nyingi kutoka makao makuu ya wilaya.
Kila kona sasa ina simulizi mpya ya kutoka giza hadi mwanga, kutoka kutazama maisha hadi kuyaendesha, kutoka uchumi wa kujikimu hadi uchumi wa kuzalisha. Mkoa wa Ruvuma una wilaya tano; Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
Kijiografia, ni mkoa mpana wenye misitu minene, milima, mabonde na vijiji vinavyotawanyika kama visiwa vilivyotenganishwa na umbali. Hali hiyo kwa miaka mingi ilifanya upatikanaji wa huduma za msingi kuwa changamoto na moja ya changamoto kubwa zaidi ilikuwa nishati ya uhakika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), safari hiyo ya giza sasa ni historia. Kwamba, vijiji vyote 554 vya Mkoa wa Ruvuma sawa na asilimia 100 vimefikiwa na umeme. Hii ni hatua ya kipekee katika ramani ya maendeleo ya Tanzania.
Mafanikio hayakuishia hapo kwani vitongoji 2,056 kati ya 3,762 tayari vimeunganishwa na gridi ya umeme katika Mkoa wa Ruvuma sawa na asilimia 54.6 ya vitongoji vyote. Hata hivyo, safari bado inaendelea kufikia asilimia 45.4 iliyosalia, jambo linaloonesha kuwa kazi ya kusogeza huduma kwa kila mwananchi bado ni kipaumbele.
Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wastani wa kaya zilizounganishwa na umeme vijijini mkoani Ruvuma umeongezeka kutoka asilimia 34 mwaka 2016 hadi asilimia 78 mwaka 2025 likiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 44 ndani ya kipindi cha miaka tisa.
Hii inamaanisha kuwa, ndani ya nyumba 10 za kijijini, karibu nane sasa zinapata mwanga, zinachaji simu bila kutegemea sola, zinatumia mashine kurahisisha uzalishaji. Watoto pia sasa wanasoma hata usiku bila moshi wa chemli au kibatali na hivyo, kuwa na uhakikika wa kutoathiri vibaya afya zao.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma, Eusebius Mhelela anasema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji wa kimkakati wa zaidi ya Sh bilioni 146. Fedha hizo zilitumika kujenga na kusambaza miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme hadi pembezoni kabisa mwa mkoa.
Mhelela anasema: “Huu si mradi wa nyaya na nguzo tu, ni mradi wa maisha mapya. Vijana wanatumia umeme kufungua gereji, mamalishe wanatumia mashine kusaga na zahanati zinahifadhi dawa na chanjo kwenye ajokofu. Haya ni mageuzi ya kweli.”
Mamalishe, vijana na wazee wote wana ushuhuda wa mabadiliko hayo. Miongoni mwa wanawake wengi wa vijijini waliob- adilishiwa ratiba ya maisha baada ya ujio wa nishati hiyo ya umeme, yumo Mary Nduguru (47) mkazi wa Kijiji cha Litembo wilayani Mbinga.
Anakumbuka kwa uchungu siku ambazo alilazimika kusaga mahindi kwa mkono, akitumia nguvu nyingi kwa uzalishaji mdogo. Wakati mwingine, alitumia mashine za dizeli zilizokuwa zinatoza gharama kubwa huku zikitoa unga mdogo kwa sababu ya uwezo mdogo wa mashine hizo.
Sasa, Mary anasimama pembeni mwa mashine yake ya umeme, mikono ikiwa na vumbi la mahindi na uso ukiwa na tabasamu la ushindi. Anasema: “Sasa nasaga kilo 300 kwa siku moja. Faida imeongezeka mara tatu…” Katika Kijiji cha Ligera kilichopo wilayani Namtum- bo, kijana Juma Mbilinyi (26) anazungumza kwa kujiamini tofauti na umri wake una- vyoonesha.
Yeye ni fundi simu, kazi ambayo miaka ya nyuma haikuwa na tija kubwa kwa sababu ya ukosefu wa nishati ya uhakika. Juma alianza kazi yake kwa kutumia sola kuchaji simu za wateja wake kwa Sh 200 kwa simu moja, kipato kilichokuwa kidogo ukilinganisha na juhudi alizoweka sambamba na muda uliotu- mika.
Lakini baada ya Ligera kuunganishwa na umeme, Juma amepata uwezo wa kuchaji simu 50 kwa siku kwa sh 500 kila moja. Ameongeza huduma za matengenezo ya simu kwa kutumia vifaa vinavyohitaji umeme na sasa anasema: “Kipato changu kimepanda kutoka kama Shilingi 150,000 hivi hadi kama 650,000 hivi wa mwezi.”
Kwa vijana wengi wa Ruvuma, simulizi ya Juma ni mfano wa namna fursa zinavyoongezeka pale nishati ya umeme inapopatikana na kuwa ya uhakika. Kwa upande wa wa- zee, mwanga huu umeleta maarifa na usalama. Katika Kijiji cha Mbati wilayani Tunduru, Mohamed Hassan (62) anakiri kuwa giza liliwahi kuwa utaratibu wa maisha yake.
“Tulikuwa tunalala mapema si kwa kupenda, bali kwa kulazimishwa na giza. Leo tunaangalia habari kwenye televisheni, watoto wanasoma usiku na usalama wa kijiji umeongezeka. Mwanga huu umetuletea maarifa,” anasema.
Mbali na maisha ya nyumbani, uchumi wa Mkoa wa Ruvuma unaendelea ku- panuka kwa kasi kutokana na kuenea kwa nishati hiyo. Ruvuma ni mkoa wenye utajiri wa rasilimali asilia ikiwemo migodi ya madini kama makaa ya mawe na urani.
Mkoa huo una mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama kahawa, korosho, tumbaku na pia kuna vikundi vingi vya usindikaji vinavyoendesha viwanda vidogo. Sekta hizi zote zinahitaji nishati ya uhakika ili kuzalisha kwa tija na kushindana katika soko.
Mwalimu mstaafu, Frank Komba mkazi wa Kijiji cha Kihagara wilayani Nyasa anasema umeme umeleta matokeo chanya moja kwa moja katika pato la wananchi wa chini. “Leo wakulima hawa- tegemei tena usafiri wa mazao yao mchana pekee. Wanatumia mashine za kusindika, wanakoboa na kusaga kwa tija na bidhaa zao zinafika sokoni zikiwa na ubora,” anasema Komba.
Ili kuimarisha zaidi huduma za nishati kwa uzalishaji mkubwa, serikali pia inaendelea na ujenzi wa njia ya msongo wa Kilo- voti 220 kutoka Songea hadi Tunduru. Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 150.78 unatarajiwa kuongeza uhakika wa umeme, kupunguza upotevu wa nishati katika njia na kuimarisha usambazaji katika viwanda na miradi ya kimkakati.
Maendeleo hayo yote yanasimamiwa ndani ya misingi ya sera na sheria za kitaifa. Sera ya Nishati ya Taifa inasisitiza upatikanaji wa umeme kwa maendeleo ya kiuchumi ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla huku Sheria ya Umeme ya Mwaka 2008 ikiipa Tanesco mamlaka ya kusimamia ugavi na ulinzi wa miundombinu ya umeme.
Aidha, Sheria ya REA ya Mwaka 2005 inalenga kuharakisha usambazaji wa nishati vijijini kwa ufad- hili wa serikali na wadau wa maendeleo. Mbali na hayo, kanuni za uharibifu wa miundombinu ya umeme zinaweka adhabu kwa yeyote atakayehusika na uharibifu wa nguzo, nyaya au vifaa vya usambazaji. Sheria hizo zimefanya miundombinu hiyo kuwa salama zaidi na kudumu kwa manufaa ya wananchi.
Lakini hata sheria zinapokuwa imara, nguvu ya kulinda mwanga huu ipo pia mikononi mwa wananchi wenyewe. Ndiyo maana Tanesco imeanzisha kampeni ya ‘Linda Nguzo, Linda Maisha’.
Kampeni hiyo inahamasisha wananchi kuripoti vitendo vya wizi wa nyaya, uharibifu wa nguzo na matumizi holela ya miundombinu ya umeme. Umeme mkoani Ruvuma ni daraja la kutoka uchumi wa kujikimu hadi uchumi wa kuzalisha. Ruvuma imethibitisha kuwa maendeleo hayaanzii mijini tu, bali popote penye nishati.
