Chanzo cha picha, MITANDAO
Mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zinazidi kushika kasi. Ni uchaguzi ambao Watanzania watamchagua rais wa Jamhuri ya Muugano, wabunge, madiwani na upande wa Zanzibar, watachagua rais, wawakilishi na nafasi sawa na za Tanzania bara.
Huu ni uchaguzi wa saba tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Lakini ndio wa kwanza kwa chama tawala CCM, kuweka mgombea mwanamke, ambaye anatarajiwa kuwa rais wa sasa Samia Suluhu Hassan.
Tangu Bunge la 12 la Tanzania kukamilisha rasmi shughuli zake tarehe 27 Juni 2025. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kumesheheni picha za watia nia hasa katika nafasi ya Ubunge – na watia nia wengi wanaonekana kuelekea chama tawala.
Watia nia wako makundi mawili; wale ambao wamezoeleka kuonekana katika shughuli za kila siku za Chama cha Mapinduzi (CCM), na hakuna anayefumbua mdomo akisikia wanataka kugombea ubunge. Kundi la pili, ni watia nia ambao hawana kabisa historia ya kujishughulisha na shughuli za wazi za CCM.
Kwanza ieleweke kwamba kuchukua fomu ya kugombea uongozi wa kisiasa ni haki ya kila anayekidhi vigezo, kupitia chama chochote kile atakacho. Lakini hilo, linakwenda sanjari na ukweli kwamba kuzijadili siasa vilevile ni haki ya kila mtu.
Takwimu zinasemaje?
Chanzo cha picha, Daily News
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, wanachama 5,475 wamechukua fomu kuwania nafasi za Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.
Baada ya kufungwa kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya CCM, kwa nafasi ya ubunge katika majimbo yote 272 ya uchaguzi nchini: Watia nia kutoka Tanzania Bara wapo 3,585. Watia nia kutoka Zanzibar ni 524. Kwa upande wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, jumla ya wagombea 503 wamechukua fomu. Kwa ujumla wagombea wa ngazi zote wakiwemo udiwani, wanafikia 20,000.
Makalla ameeleza, idadi hiyo inaonesha mwitikio mkubwa wa wanachama wa CCM katika kushiriki kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama, na hatua inayofuata ni mchakato wa uchujaji.
Kwa nini wanakimbilia CCM?
Chanzo cha picha, MITANDAO
Jawabu ya swali hili, litategemea unamuuliza nani. Bila shaka CCM itasema ni dalili ya kukubalika kwao. Chama ni kikongwe na kimejipanga. Hoja hiyo itatiliwa mkazo na ushawishi ambao bado chama hicho kinao ndani ya siasa za Tanzania.
Ingawa wapinzani wao wanaweza kujenga hoja kuwa, wengine wanakimbilia CCM kwa sababu ya kutegemea mteremko. Hoja hii itatiliwa mkazo na kile kilichotokea katika uchaguzi wa 2020. CCM ilipopata ushindi mkubwa wenye utata katika ngazi zote za udiwani, ubunge na uwakilishi. Ingawa CCM wenyewe pamoja na Tume ya Uchaguzi wakati huo (NEC) ilisisitiza uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Mbali na jawabu hizo, kuna jawabu la tatu la swali hili. Nilipomuliza mchambuzi wa siasa za Tanzania, Thomas Kibwana, kwa nini kuna idadi kubwa ya watia nia wanaokimbilia CCM?
“Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakijasaini fomu za maadili kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu mpaka sasa, kwa hiyo huenda wapo baadhi ya watu ambao labda wangegombea kupita Chadema, lakini wameamua kutafuta vyama vingine. Wengine tumewaona wakienda Chaumma na ACT Wazalendo, na wengine ndio hao wanakwenda CCM.”
Kilichotokea 2020
Miongoni mwa Wabunge wa mwanzoni ambao walitangaza kuihama Chadema na kuhamia CCM, alikuwa ni Mbunge wa jimbo la Siha Mkoani Kilimanjaro kupitia chama hicho, Dkt Godwin Mollel, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa jimbo hilo hilo lakini kupitia CCM tangu 2020, pia ni Naibu Waziri wa Afya.
Mwezi Oktoba 2018, akinukuliwa na vyombo vya habari, alisema hajutii uamuzi wake wa kuondoka Chadema. Fauka ya hilo, pia alisema, “nimesikia wataondoka wabunge karibia wote na watabaki kumi, na wakati wa uchaguzi atashinda mbunge mmoja ambaye kwa sasa siwezi kumtaja.”
Alichokisema Dkt. Mollel ndicho kilichotokea. Baada ya uchaguzi wa 2020 kukamilika, ni kweli Chadema ilipata Mbunge mmoja tu aliyeshinda kwa kuchaguliwa, Aida Khenani katika jimbo la Nkasi Kaskazini, mkoani Rukwa.
Katika uchaguzi wa 2020, kuna mambo makubwa mawili yalitokea na kuleta mshangao mkubwa. Mosi, kulikuwa na idadi kubwa ya wabunge na madiwani wa CCM ambao walipita bila kupingwa. Pili, CCM ilibeba ushindi wa kishindo ulioibua mjadala, hadi katika majimbo ambayo ni ngome za vyama vya upinzani.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Mwananchi, hadi Aprili 2023, Bunge la Tanzania lilikuwa na wabunge 28 waliopita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa 2020, wakiwemo mawaziri kadhaa na wabunge.
Mwezi Machi 2023, Mahakama Kuu Tanzania ilitoa hukumu ya kuzuia wagombea wa nafasi mbalimbali kupita bila kupingwa katika chaguzi zinazofanyika. Hukumu hiyo ilitokana na kesi namba 19 ya 2021 iliyofunguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Joran Bashange.
Kwa upande wa CCM wameonekana kukubaliana na hukumu hiyo. Kwa nyakati tofauti viongozi wa chama hicho wamenukuliwa wakisema, hakutakuwa na kupita bila kupingwa katika uchaguzi ujao.
Mwezi Machi 2025, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, akizungumza katika Wilaya ya Ileje, alieleza chama hicho kimeweka utaratibu wa wazi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na hakutakuwa na utaratibu wa wagombea kupita bila kupingwa.
Kauli hii inalindwa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, ambayo imeongeza takwa la mgombea kupigiwa kura ya ndiyo au hapana kama amebaki peke yake, wengine wameondolewa ama amejitokea mgombea mmoja pekee kuwania nafasi husika, lakini si kupita bila kupingwa.
Pamoja na Sheria hii, utitiri wa wagombea hawa, unaendelea kutazamwa kwa utaratibu wa ndani ya chama ili kupata mgombea mmoja wa kila jimbo kuwakilisha CCM. Safari ya wagombea ndani ya chama, inaanzisha safari ya wagombea kwenye uchaguzi mkuu. Lakini swali kubwa hapa, Je, uchaguzi wa 2025 utatoa uhuru na haki kamili kupitia sanduku la kura?