Geita. Kampuni za uchimbaji wa madini nchini zimetakiwa kuwawezesha wachimbaji wadogo katika teknolojia za kisasa na usimikaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kujenga uchumi jumuishi unaotokana na sekta ya madini.

Wito huo umetolewa leo Jumapili, Februari 22, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Amesema mgodi huo umezalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 2,366 moja kwa moja na 4,629 kupitia wakandarasi mbalimbali wanatoa huduma katika mgodi wa GGML.

Ameutaka uongozi wa mgodi huo kuhakikisha shughuli zake zinakuwa na athari chanya katika uchumi wa jamii zinazowazunguka kwa kutoa fursa za kazi za muda mfupi ikiwemo kuwezesha miradi mbalimbali ya kijamii.

Sambamba na hilo, ameipongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), kwa kusimamia sheria na kuhakikisha kampuni hiyo inazingatia usalama wa wafanyakazi wake.

“Pongezi hizi inastahili OSHA ambayo imekuwa ikiwaongoza katika kutekeleza hayo kupitia usimamizi mzuri wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na miongozo mbalimbali chini ya sheria hiyo ambayo wamekuwa wakiitoa kupitia kaguzi zao za mara kwa mara,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amesema OSHA ni miongoni mwa taasisi zenye msaada mkubwa katika kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika kwa tija katika Mkoa wa Geita.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema ziara hiyo, inalenga kuona jinsi OSHA inavyoshirikiana na wadau wake kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambayo dhima yake kuu ni kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi pamoja na kulinda uwekezaji kupitia kuzuia uharibifu wa mali.

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita, Menejimenti ya Mgodi wa Geita na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).

Awali, menejimenti ya GGML iliwasilisha taarifa juu ya shughuli zao iliyoainisha jinsi afya na usalama wa wafanyakazi unavyozingatiwa katika shughuli husika.

Miongoni mwa masuala yaliyoelezwa katika taarifa hiyo ni pamoja na historia ya mgodi ambapo imeelezwa kuwa madini katika mgodi huo yaligunduliwa mnamo mwaka 1898 na uchimbaji rasmi kuanza mwaka 1999.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *