Chanzo cha picha, Dira
Katika taifa linalohitaji mabadiliko yoyote, vyama vya siasa vikiwepo vya upinzani huwa na nafasi ya kipekee. Nchini Tanzania vyama vya upinzani ambavyo vilitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi sasa vinaonekana kugawanyika kuliko wakati wowote ule.
Badala ya mijadala ya sera na hoja mbadala dhidi ya watawala, kwa miezi kadhaa sasa, tunashuhudia majibizano na mashambulizi ya moja kwa moja baina ya vyama vya upinzani badala ya kuunga nguvu zao zaidi dhidi ya chama tawala, CCM.
Vita vya maneno kuanzia ya majukwaani hadi kwenye mitandao ya kijamii vimechukua nafasi ya mijadala ya sera mbadala dhidi ya chama tawala.
Kisiasa tunashuhudia kile ambacho wakili na mtaalamu wa haki za binadamu Fortunata Kitokesya anakieleza kama “theatre of ego” ama jukwaa la ubinafsi, na sio jukwaa la matumaini.
Aidha, maswali mengi yanajielekeza kwenye kujua kwanini ‘wanazodoana’ wakati huu? nini kimetokea na je vyama hivi vya upinzani ama upinzani kwa ujumla unajimaliza na kujizika wenyewe taratibu?
Vita baridi ya CHADEMA vs ACT
Kwa muda sasa, kuna mvutano mkubwa unaoendelea hadharani kati ya vyama viwili vikuu vya upinzani Tanzania, CHADEMA na ACT Wazalendo.
ACT ina ngome imara Zanzibar na ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ikitoa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo. CHADEMA, kwa upande mwingine, kama chama kikuu cha upinzani Tanzania, kina historia ndefu ya harakati za kisiasa, kikiwa na nguvu upande wa bara.
Hata hivyo kuna vyama vingine ambavyo havipaswi kupuuzwa kama CUF, NCCR Mageuzi na sasa CHAUMMA ambacho kimeanza kupata nguvu baada ya baadhi ya viongozi waliokuwa CHADEMA kujiunga nacho kupitia kundi la G-55. Ingawa kuna vita ya kushambuliana isiyopuuzwa ya CHAUMMA na CHADEMA, lakini maneno ya hadharani kati ya CHADEMA na ACT yana picha tofauti.
Kama mgeni kabisa wa siasa za Tanzania, unaweza kufikiri ni vita ya vyama visivyo upande mmoja wa upinzani.
Leo hii ndani ya upinzani, kuna kile kinachoitwa “upinzani wa upinzani.” Viongozi na makada wake hasa wa vyana vya CHADEMA na ACT-Wazalendo wanarushiana maneno hadharani badala ya kujikita zaidi kwenye hoja dhidi ya chama tawala. Lakini nini chanzo cha mvutano wao?
Chanzo cha picha, Mwanahalisi
Nini chanzo cha malumbano ya wapinzani?
Chanzo kikuu cha mvutano wa sasa ni tofauti ya msimamo kuhusu uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 2025. CHADEMA imetangaza msimamo wake kupitia No Reforms No Election ikisema haitashiriki uchaguzi wowote usiofanyika chini ya mazingira huru na haki.
Kwa upande mwingine, ACT-Wazalendo na vyama vingine kama NCCR-Mageuzi, CUF na sasa Chaumma wamesisitiza kuwa wataendelea kushiriki uchaguzi huo ili “kupambana ndani ya uwanja,” wakiamini mabadiliko hayawezi kusubiri mazingira kuwa bora.
CHADEMA imewataja wanaoshiriki uchaguzi kuwa “wamekubali kutumika na mfumo.” Wengine wanatafsiri hatua hiyo kama usaliti kwa harakati za kudai tume huru ya uchaguzi. Kwa upande wao, ACT wanadai kuwa CHADEMA inatafuta huruma ya kisiasa kwa kugomea mchakato ambao hauwezi kusimamishwa.
Mzozo huo umegeuka kuwa mashambulizi binafsi kwenye mitandao ya kijamii, kila upande ukitafuta kuhalalisha msimamo wake huku ukidhoofisha ule wa mwingine. Viongozi wameanza kutumia maneno makali hadharani.
“Takataka”
Chanzo cha picha, Zitto
ACT Wazalendo kinawaona CHADEMA kama walioamua kususia uchaguzi. Mmoja wa waasisi wake Zitto Kabwe anasema “Kususia uchaguzi ni kuwapa ushindi CCM ” akihoji mbinu mbadala zinazopendekezwa na wanaosusia: “Waseme watatumia njia gani kuzuia uchaguzi.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, ameenda mbali zaidi kwa kuandika kwenye X (zamani Twitter): “Kwanini tusidhani waliosusa wamehongwa na CCM?” Alihoji Nondo na kuendelea kusema: “Hatususi uchaguzi oktoba, tutalinda kura zetu”.
Kauli hizo zimejibiwa na CHADEMA. John Heche, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, aliwajibu ACT-Wazalendo kwa kusema: “Kifungu cha 92 cha sheria mpya ya uchaguzi kinasema Mkurugenzi anaweza kuamua wapi kura zihesabiwe. Kura zimepigwa Manga, zinahesabiwa Sirari. Huwezi kulinda kura zilizoibiwa na sheria na kanuni kabla ya kupigwa.”
Kwenye chapisho lake kupitia mtandao wa X, Heche alitupa kijembe kwa ACT kwamba watawezaje kuidhibiti na kuishinikiza CCM kufanya mabadiliko hata kwa ahadi ya ‘kupewa’ wabunge watatu?
Zitto Kabwe alijibu kwa neno moja tu: “Takataka.” Jibu hilo lilizua mjadala zaidi kuhusu namna viongozi wa kisiasa hao wa upinzani wanavyowasiliana hadharani.
Kwa wengi, hili lilikuwa ishara kwamba mawasiliano ya kisiasa sasa yameporomoka na hayaonyeshi dalili ya upinzani kuimarika dhidi ya CCM bali upinzani kuimarika dhidi ya upinzani.
Mwananchi mmoja aliandika kwenye X: “Upinzani hawana vita ya hoja kwa Chama Cha Mapinduzi. Kilichobaki ni vita vya hoja wenyewe kwa wenyewe.”
Fortunata Kitokesya anatahadharisha kuwa iwapo hali hii itaendelea, wananchi wataendelea kupoteza imani na vyama vya upinzani.
Vita yao kicheko kwa CCM
Chanzo cha picha, CCM
Katika uchaguzi mkuu wa 2015 kulikuwa na muungano wa vyama vya upinzani vikubwa vya CHADEMA, NCCR- Mageuzi, CUF na kingine ‘kidogo’cha NLD chini ya mwavuli wa UKAWA.
Mgombea wa urais kupitia muungano huo, Lowassa alipata kura 6.07 milioni zilizovunja rekodi kwa upinzani, kura nyingi zaidi kuliko alizopata Jakaya Kikwete wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, ambaye alipata kura milioni 5.27na kushinda urais.
Vyama hivyo pia vilizoa idadi kubwa ya wabunge kupata kutokea kwenye siasa za upinzani nchini Tanzania. Kwa pamoja vilizoa wabunge 116 wakiwepo wa viti maalumu. Katika uchaguzi huo wa mwaka 2015, CHADEMA ilifikisha wabunge 70 kutoka wabunge 48 waliopata kwenye uchaguzi wa 2010, CUF walizoa wabunge 45 kutoka 36 mwaka 2010, na NCCR ilipata mbunge mmoja.
Mazingira ya uchaguzi wa 2020 yalikuwa tofauti kabisa kuweza kupima nafasi ya vyama vya upinzani Tanzania. Lakini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, kila chama sasa kimejichimbia kwenye msimamo wake. Lakini msimamo tu sio jambo la ajabu sana, ila la kustaajabisha ni namna wanavyopambana wao kwa wao hadharani wakati ambao uchaguzi mkuu ukiwa mlangoni.
Vipo vyama 14 vya upinzani vilivyotangaza mwezi uliopoita kuangalia namna ya kushiriki kwa pamoja katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025. Vyama hivyo ni CUF, NCCR, NLD, DP, NRA, UDP, MAKINI, CCK, UPDP, SAU, TLP, AAFP na UMD. Pamoja na kuungana huko, wanapingwa na CHADEMA. CHADEMA wanaviona vyama hivi vya upinzani kama vyama ‘pandikizi’ vilivyoKO kimkakati kuIsaidia chama tawala.
Hata hivyo hilo linapingwa na katibu wa AAFP, Rashid Rai. ‘Kuna kauli kuwa vyama hivi ni chawa, mamluki, mapandikizi, haya ni maneno yaliyozungumzwa kwa miaka mingi, lakini nataka kuwaambia kuwa kwa mara ya kwanza kinakwenda kutokea kishindo katika uchaguzi Mkuu wa 2025’.
Wakati vyama vya upinzani vinapingana hadharani, CCM chama tawala kimekaa pembeni kikitazama. Hakihitaji kujibu lolote, kwa sababu wapinzani wake wameamua kupambana wao kwa wao.
Kwa mujibu wa The Chanzo walioripoti tafiti za REPOA, kwamba asilimia 59 tu ya wananchi ndio wanaoamini vyama vya siasa, CCM na upinzani kwa pamoja. Lakini ni asilimia 10 tu ya Watanzania ndio wanaosema wanaamini vyama vya upinzani peke yao. Hii inaonesha wazi kuwa upinzani ndani ya upinzani unaoendelea unazidi kuharibu imani iliyobaki kwao.
Katika mazingira kama haya, ni rahisi kwa CCM kuendelea kuimarisha nafasi yake mbele ya baadhi ya wananchi waliokatishwa tamaa na siasa za upinzani. Ukiacha mazingira mengine ya kisiasa yaliyopo, upinzani ndani ya upinzani utaendelea kuinufaisha CCM huku upinzani ukiendelea kujiua taratibu taratibu.