Mtu mwenye silaha amefyatua risasi Jumatano, Agosti 27, katika kanisa moja huko Minneapolis, Minnesota, karibu na shule, na kuua angalau watoto wawili na kuwajeruhi wanafunzi wengine 14 waliokusanyika kwa Misa, polisi imesema. Mshukiwa huyo ambaye alitekeleza kitendo hicho akiwa peke yake, alijiua katika eneo la tukio.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mauaji hayo yalitokea katika kanisa lililo karibu na shule ya Minneapolis, ambapo wanafunzi walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya Misa kusherehekea mwanzo wa mwaka wa shule. Mshambuliaji, mwenye umri wa miaka ishirini, alikuwa amebeba bunduki tatu. Alijiua katika eneo la shambulizi, Mkuu wa Polisi wa Minneapolis Brian O’Hara amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

“Watoto wawili wadogo wenye umri wa miaka 8 na 10 waliuawa wakiwa wamekaa kwenye viti,” Brian O’Hara ameeleza na kuongeza kuwa watu 17 walijeruhiwa, wakiwemo watoto 14 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 15. Waumini watatu wa parokia walio na umri wa zaidi ya miaka 80 pia walijeruhiwa. Kulingana na Brian O’Hara, majeruhi wanaedelea vizuri.

FBI inafungua uchunguzi kuhusu “uhalifu wa chuki dhidi ya Wakatoliki”

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, mshambuliaji ametambuliwa kama Robin Westman, 23. Ripoti hizi za vyombo vya habari zinataja nyaraka za mahakama za mwaka 2019-2020 ambazo zinaripoti mabadiliko ya jina la kwanza kutoka kwa Robert hadi Robin kwa mtu huyu, ambaye alizaliwa kiume lakini akatambuliwa kama mwanamke. Kulingana na wachunguzi, mtu huyo alifyatua risasi kadhaa kwa kutumia bunduki mbili na bastola moja.

Ofisi ya Upelelezi ya Marekani (FBI) imefungua uchunguzi kuhusu “ugaidi wa ndani” na “uhalifu wa chuki dhidi ya Ukatoliki,” ametangaza Kash Patel, mkuu wa shirika hilo. Mshambuliaji alikuwa mwanafunzi wa zamani katika shule hiyo, ameongeza. Mkuu wa Polisi wa Minneapolis Brian O’Hara amesema mshambuliaji alikuwa ametayarisha waraka ambao ungechapishwa baadaye kwenye tovuti ya kushiriki video ya YouTube. Polisi “wameuondoa”.

Daktari katika Hospitali ya Hennepin Healthcare amesema aliwatibu wagonjwa 11, wakiwemo watu wazima wawili na watoto tisa. Wanne kati yao walihitaji upasuaji wa dharura. “Ninawaombea watoto wetu na walimu, ambao wiki yao ya kwanza shuleni iliharibiwa na kitendo hiki kibaya cha vurugu,” Gavana wa Minnesota Tim Walz ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

“Shambulio lisilo na maana”

“Hiki kilikuwa kitendo cha makusudi cha ukatili dhidi ya watoto wasio na hatia na wengine waliofika kuabudu. “Ukatili na vitisho katika kanisa lililojaa watoto havieleweki kabisa. Mioyo yetu imevunjika kwa familia zilizopoteza watoto wao, kwa maisha haya ya vijana wanaotatizika kuishi, na kwa wakazi walioumizwa na shambulio hili lisilo na maana,” ameongeza mkuu wa polisi, akibainisha kuwa uchunguzi unaendelea.

Marekani ina kiwango cha juu zaidi cha vifo vinavyohusiana na bunduki kuliko nchi yoyote iliyoendelea. Ufyatulianaji wa risasi ni janga la mara kwa mara ambalo serikali zilizofuata hadi sasa zimeshindwa kukomesha, huku Wamarekani wengi wakisalia kushikamana, huku raia wengi wakimiliki silaha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *