#HABARI: Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutatua changamoto za ardhi na kuendeleza programu za maridhiano kati ya wakulima na wafugaji, ili kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu wilayani Kilosa na maeneo jirani.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika, Agosti 30, 2025, mjini Kilosa mkoani Morogoro, Dkt. Samia amesema tayari serikali kupitia Wizara ya Ardhi imefuta mashamba yasiyoendelezwa na kupanga matumizi upya kwa manufaa ya wananchi.
Amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya hekari 53,000 zimefutwa milki zake, ambapo hekari 21,872 zimepimwa na kugawiwa kwa matumizi ya kilimo, makazi na uwekezaji. Hatua hiyo imewanufaisha wananchi 8,557 kutoka vikundi 186 katika vijiji 11 vya wilaya hiyo.
“Niwahakikishie, tutatagawa bila kumuonea mtu, bila dhuluma, na wale wenye shida tunawatambua, watapata vipande vya ardhi,” ameongeza Dkt. Samia huku akiahidi kukamilisha zoezi hilo baada ya kurejea madarakani.
Akizungumzia migogoro kati ya wakulima na wafugaji, Dkt. Samia amesema CCM imepanga kuendeleza programu ya Tutunzane, ambayo imeleta mafanikio katika wilaya ya Mvomero kwa kuimarisha mshikamano na mshikiano baina ya pande mbili hizo.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania #uchaguzimkuu2025